Hashdu Sha'abi Iraq: Tupo tayari kwenda kuisafisha Syria kutokana na Daesh
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i29794-hashdu_sha'abi_iraq_tupo_tayari_kwenda_kuisafisha_syria_kutokana_na_daesh
Msemaji wa Harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi nchini Iraq, ameelezea utayarifu wa wapiganaji wake kwa ajili ya kupambana na genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh ndani ya ardhi ya Syria kupitia ushirikiano kamili wa serikali ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 30, 2017 03:57 UTC
  • Hashdu Sha'abi Iraq: Tupo tayari kwenda kuisafisha Syria kutokana na Daesh

Msemaji wa Harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi nchini Iraq, ameelezea utayarifu wa wapiganaji wake kwa ajili ya kupambana na genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh ndani ya ardhi ya Syria kupitia ushirikiano kamili wa serikali ya nchi hiyo.

Karim al-Nuri sambamba na kuelezea mafanikio yaliyofikiwa katika mapambano na kundi la kigaidi la Daesh mjini Mosul, kaskazini mwa Iraq amesema kuwa, wanamapambano wa Hashdu sh-Sha'abi wanaendelea na operesheni hizo na kwa sasa wamefika katika mpaka wa Syria na Iraq.

Wanamapambano wa Hashdu sh-Sha'abi 

Al-Nuri ameyasema hayo katika mazungumzo na kanali ya televisheni ya al-Mayadin ya nchini Lebanon na kuongeza kuwa, baada ya wapiganaji wa harakati hiyo kufika katika mipaka ya Syria, ni rahisi sana kuweza kuingia maeneo ya Raqqa, kaskazini mwa Syria. Aidha msemaji wa harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi nchini Iraq ameongeza kuwa, hatua ya wapiganaji wa harakati hiyo kufika maeneo ya mpaka wa Syria, inaashiria kufikia mwisho uhai wa kundi la Daesh (ISIS.) Naye kwa upande wake Hadi al-Aamir, Katibu Mkuu wa Idara ya Badr ya nchini Iraq sambamba na kuthibitisha kufika wanamapambano wa Hashdu sh-Sha'abi katika mpaka wa Syria na kujiandaa kuingia ardhi ya nchi hiyo kuwasaka magaidi wa genge hilo hatari la Daesh, ameitaka Damascus kutoa idhini na ushirikiano kamili na kwamba harakati hiyo haitofanya lolote bila kuwepo makubaliano ya pande mbili.

Hashdu sh-Sha'abi  ikizidi kusonga mbele kuwasaka magaidi wa Kiwahabi

Kabla ya hapo pia al-Aamiri alinukuliwa na Shrikika la Habari la Sputnik akisema kuwa, serikali ya Syria imeitaka Hashdu sh-Sha'abi kuingia ardhi ya nchi hiyo baada ya kusafishwa kikamilifu ardhi ya Iraq kutokana na uepo wa magaidi hao. Inafaa kuashiria kuwa, harakati hiyo inatambuliwa na Wairaqi kuwa na umuhimu mkubwa katika operesheni za kukombolewa maeneo tofauti ya nchi hiyo hususan Mosul.