Kaburi la umati lenye miili 60 lagunduliwa magharibi mwa Mosul, Iraq
Vikosi vya serikali ya Iraq vimegundua kaburi la umati lenye miili 60 ya raia waliouliwa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) magharibi mwa mji wa Mosul.
Duru za habari zimeliarifu shirika la habari la al-Sumaria kuwa, kaburi hilo limegunduliwa katika wilaya ya al-Shifa, magharibi mwa Mosul, eneo lililokuwa likishikiliwa na magaidi wa Daesh.
Habari zaidi zinasema kuwa, maiti za wazee na wanawake 23 ni miongoni mwa miili hiyo 60 iliyokuwemo kwenye kaburi hilo la umati. Vyanzo vingine vya habari vimeripoti kuwa, miili hiyo imehamishiwa eneo la Wadi Hajar kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na utambulisho.
Aghalabu ya miili hiyo imeripotiwa kuwa na majeraha ya risasi kichwani, mbinu inayotumiwa na magaidi hao wakufurishaji wanapofanya jinai na mauaji ya umati.
Makuburi kadhaa ya umati yamegunduliwa katika maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na wakufurishaji wa Daesh, tangu jeshi la Iraq lilipoanzisha operesheni ya kuukomboa mji huo kutoka kwenye makucha ya mgaidi hao mwezi Oktoba mwaka 2014.
Hivi karibuni, shirika la kutetea haki za bindamu la Human Rights Watch (HRW) liliripoti kuwa kundi la kigaidi la Daesh limeua mamia ya mahabusi wakiwemo maafisa usalama wa Iraq katika mji wa Mosul na kuwazika katika kaburi la umati ambalo yumkini likawa kubwa zaidi ya makaburi yote ya umati yaliyogunduliwa nchini Iraq hadi hivi sasa.