Israel yakiri kuwapa matibabu magaidi wanaojeruhiwa nchini Syria
Afisa mmoja wa utawala wa Kizayuni wa Israel amekiri kuwa, jeshi la utawala huo linawapa matibabu magaidi na wapinzani wa serikali ya Syria ambao wanajeruhiwa vitani nchini Syria na kuutaja msaada huo kuwa eti ni 'kazi takatifu zaidi'.
Kwa mujibu wa gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post, Kapteni Aviad Camisa, Naibu Mkuu wa Kitengo cha Matibabu katika Divisheni ya 210 ya Bashan, amekiri wazi wazi kuwa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limekuwa likiwapa matibabu kwa magaidi kutoka Syria. Amesema magaidi hao wanatibiwa katika Miinuko ya Golan ya Syria ambayo sasa inakaliwa kwa mabavu na Israel. Camisa amesema, Israel hutoa huduma bora, za haraka na za kisasa kabisa kwa magaidi waliojeruhiwa vitani nchini Syria.

Hadi hivi sasa zaidi ya magaidi 3,000 waliojeruhiwa vitani Syria wamepata matibabu katika hospitali za utawala wa Kizayuni wa Israel na baada ya kupona hurudishwa tena kuendeleza vita dhidi ya serikali halali ya Syria.
Tokea mgogoro wa Syria uanze mwaka 2011, utawala haramu wa Israel umekuwa ukitoa msaada wa kitiba, kijeshi na kilojistiki kwa magaidi wanaotaka kuiangusha serikali ya Rais Bashar al Assad. Israel imekuwa ikifanya mashambulizi ya angani Syria kwa ajili ya kuwaunga mkono magaidi hao wakiwemo wa ISIS au Daesh, Jabhat Al Nusra n.k.