Kubariki Umoja wa Mataifa njama zinazotekelezwa na Saudia nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i30042-kubariki_umoja_wa_mataifa_njama_zinazotekelezwa_na_saudia_nchini_yemen
Harakati ya Ansarullah ya Yemen imekosoa pendekezo la mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu kukabidhi udhibiti wa bandari ya Al-Hudayda kwa upande mwengine wa tatu usioegemea upande wowote.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 04, 2017 21:47 UTC
  • Kubariki Umoja wa Mataifa njama zinazotekelezwa na Saudia nchini Yemen

Harakati ya Ansarullah ya Yemen imekosoa pendekezo la mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu kukabidhi udhibiti wa bandari ya Al-Hudayda kwa upande mwengine wa tatu usioegemea upande wowote.

Ansarullah ya Yemen pamoja na waitifaki wake wameeleza kuwa pendekezo la Ismail Ould Cheikh Ahmed, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen kuhusiana na suala hilo ni la kutowajibika na limewavunjia heshima mamilioni ya Wayemeni.

Ansarullah na washirika wake wametangaza kuwa mtazamo wa Ismail Ould Cheikh Ahmed kuhusu sababu kuu ya kuzidi kuwa mbaya hali ya maafa inayowakabili raia wa Yemen si sahihi na wakasisitiza kwamba Umoja wa Mataifa umetoa pendekezo hilo kutokana na mamluki kushindwa kuidhibiti kijeshi bandari ya Al-Hudaydah.

Ismail Ould Cheikh Ahmed 

Ismail Ould Cheikh Ahmed amependekeza kuwa uendeshaji wa bandari ya Al-Hudaydah ukabidhiwe kwa upande wa tatu usiopendelea upande wowote au uwe chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.

Pendekezo hilo lisilo na busara la mjumbe wa Umoja wa Mataifa limetolewa katika hali ambayo bandari ya Al-Hudaydah ndiyo bandari muhimu zaidi nchini Yemen ambapo karibu asilimia 80 ya shehena za vyakula na dawa zinawafikia wananchi kupitia bandari hiyo.

Mpango huo uliopendekezwa na Umoja wa Mataifa ambao ni nuskha inayonakili hatua na mipango ambayo imetekelezwa na Saudi Arabia katika miezi ya karibuni kwa madhumuni ya kuidhibiti bandari hiyo, inajaribu kwa namna fulani kuhalalisha hatua za utawala wa Riyadh za kushadidisha mzingiro dhidi ya wananchi wa Yemen na kufanikisha malengo yake ya kubeberu ndani ya nchi hiyo.

Bandari ya Al-Hudaydah

Saudia imetumia kisingizio na madai ya kuingizwa kimagendo nchini Yemen silaha na zana za kijeshi kupitia bandari ya Al-Hudaydah ili kuligeuza eneo la bandari hiyo kuwa la kijeshi na kutaka kuifunga na hatimaye kuibomoa bandari hiyo.

Lengo la Saudi Arabia la kuitangaza bandari ya Al- Hudaydah eneo la kijeshi ni kuiondoa bandari hiyo kwenye udhibiti wa vikosi vya wananchi wa Yemen na vilevile kuiwekea mashinikizo serikali ya uokovu wa kitaifa ya nchi hiyo. Saudia inafanya juu chini, ili kwa kuifunga bandari ya Al-Hudaydah na kushadidisha mzingiro wa kiuchumi dhidi ya Yemen kuifanya serikali ya uokovu wa kitaifa ionekane kuwa ni serikali isiyo na ufanisi kiutendaji, hivyo kuweza kuandaa mazingira ya kufikia malengo yake, ambayo ni kuwarejesha madarakani vibaraka wake.

AbduRabbuh Mansur Hadi

Tangu mwezi Machi 2015, kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani na kwa kisingizio cha kutaka kumrejesha madarakani AbduRabbuh Mansur Hadi, rais wa Yemen aliyejiuzulu na kuitoroka nchi, Saudi Arabia ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen na kuizingira nchi hiyo kuanzia angani, nchi kavu na baharini. Uvamizi huo hadi sasa umesababisha maelfu ya Wayemeni kuuawa na mamia ya maelfu ya wengine kujeruhiwa.

Uvamizi na uingiliaji wa Saudia katika masuala ya Yemen unapasa kutathminiwa katika muelekeo wa uchu na tamaa ya kibeberu ambayo umekuwa nayo siku zote utawala wa Aal Saud na Magharibi kuhusiana na nchi hiyo. Kuivamia Yemen na kupora ardhi zaidi za nchi hiyo ni ajenda ambayo imekuwa ikifanyiwa kazi kila mara na Saudia. Hapo kabla Saudia ilizipora ardhi za mikoa mitatu ya Yemen ya Usair, Najran na Jizan na kuzifanya sehemu ya ardhi yake.

Uharibifu unaotokana na jinai za Saudia nchini Yemen

Lakini mbali na kufuatilia malengo ya kujitanua, utawala wa Aal Saud unatekeleza pia mpango wa Marekani wa kuigawa Yemen mapande kadhaa na kuunda serikali ya Shirikisho inayojumuisha tawala kadhaa kwa madhumuni ya kuidhoofisha na kuisambaratisha nchi hiyo. Katika hali hiyo, wafuasi wa Mansur Hadi ambao ni vibaraka na mamluki wa Saudia wanafanya kila njia ili kwa msaada wa Umoja wa Mataifa  na madola ajinabi kuandaa mazingira ya kuwakandamiza na kuwabana zaidi wananchi wa Yemen na kuyaondoa maeneo mbalimbali kwenye udhibiti wa serikali ya uokovu wa kitaifa ya nchi hiyo.

Umoja wa Mataifa, ambao umebaki kuwa mtazamaji tu wa jinai zinazofanywa na Saudi Arabia, umependekeza mpango wa kisiasa ambao lengo lake ni kutaka kuhalalisha hatua za kuigawa Yemen zinazofuatiliwa na Riyadh na madola ya Magharibi. Lakini kile ambacho umoja huo umekipuuza ni hali mbaya ya raia wanaoatilika kwa vita na waliowekewa mzingira wa Yemen ambao kutokana na athari hasi za vita hivyo wanakabiliwa na masaibu yanayoongezeka kila uchao yakiwemo maradhi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ugonjwa thakili wa kipindupindu.../