Mshauri wa Bashar al Assad: Syria haijaiacha pekee yake Palestina
Mshauri wa Rais wa Syria amesema kuwa maadui walitumia stratejia zao zote dhidi ya Syria, hata hivyo hawakufikiria kwamba Iran, Russia na Harakati ya Hizbullah zingesimama imara mbele ya stratejia hizo na kutoa pigo.
Bouthaina Shaaban ambaye ni Mshauri wa Masuala ya Siasa na Habari wa Rais Bashar al Assad wa Syria amesema katika mkutano wa Siku ya Kimataifa ya Quds huko Damascus kuwa watafanikiwa kuzima njama za maadui iwapo kutakuwa na umoja miongoni mwao. Bi Bouthaina amesisitiza kuwa utawala wa Kizayuni umekuwa ukifuatilia malengo maalumu tangu uanze kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina kukiwemo kuzusha hitilafu kati ya Waarabu na Waislamu, lakini akasema Syria imekuwa ikiendesha muqawama na kukabiliana na hatua hizo za Wazayuni.
Mshauri wa Masuala ya Siasa na Habari wa Rais wa Syria amesema kuwa, kusimama kidete na kuendesha muqawama ni nyenzo mbili kuu zitakazoupa ushindi Umma wa Kiislamu na kusambaratisha njama za maadui za kuzigombanisha nchi za Kiarabu na kuzusha mgawanyiko kati ya nchi hizo.