Amani ya kudumu hupatikana kwa ushirikiano si kwa misimamo ya Kidaesh
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i31026-amani_ya_kudumu_hupatikana_kwa_ushirikiano_si_kwa_misimamo_ya_kidaesh
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, eneo la Ghuba ya Uajemi limekumbwa na matatizo mawili makuu ya kimuundo na kutojitambua. Amesema, baadhi ya nchi za eneo hili zinaona usalama wao utapatikana kwa kununua amani kutoka nje wakati ambapo usalama wa kweli unaweza kupatikana tu kwa ushirikiano wa kieneo na kupitia nchi zenyewe za eneo hili.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 27, 2017 12:57 UTC
  • Dk Mohammed Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran
    Dk Mohammed Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, eneo la Ghuba ya Uajemi limekumbwa na matatizo mawili makuu ya kimuundo na kutojitambua. Amesema, baadhi ya nchi za eneo hili zinaona usalama wao utapatikana kwa kununua amani kutoka nje wakati ambapo usalama wa kweli unaweza kupatikana tu kwa ushirikiano wa kieneo na kupitia nchi zenyewe za eneo hili.

Dk Mohammed Javad Zarif alisema hayo jioni ya jana Jumatatu katika kikao cha kila mwaka cha uhusiano wa kigeni wa barani Ulaya huko Berlin, Ujerumani na huku akigusia vitendo vibaya vya baadhi ya nchi za eneo hili amesisitiza kuwa: Si sahihi hata kidogo kuwa na dhana ya kupata ushindi kupitia migongo ya wengine, kwani amani haiwezi kupatikana kwa kuhatarisha usalama na amani ya nchi nyingine.

Trump akitiliana saini na mfalme Salman wa Saudia, mkataba wa mabilioni ya dola

 

Amesema, amani si kitu kinachoweza kununuliwa kwa fedha na siasa za kigeni si bidhaa. Pia amesisitiza kuwa, kutiliana saini mikataba ya silaha na dola fulani hakuna maana ya kushirikishwa katika kulinda usalama. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekosoa vikali fikra inayoenezwa na Saudi Arabia ya kuwabebesha wengine lawama za matendo yake na kuongeza kuwa, miamala ya namna hiyo inafanana na ya Kidaesh. 

Ukweli wa mambo ni kuwa, siasa za mambo ya nje za Saudia zimelitumbukiza eneo la kiistratijia la Asia Magharibi katika mgogoro mkubwa. Viongozi wanagenzi wa Saudi Arabia wanazitumia siasa za mambo ya kigeni kama wenzo ya kulinda maslahi yao binafsi kupitia kuzusha maadui wa kupandikiza. Hatua ya Saudia ya kumwalika rais wa Marekani Donald Trump  kutembelea Riyadh ni ushahidi wa wazi wa ukweli kwamba viongozi wa nchi hiyo wanaamni kuwa usalama wao unapatikana nje ya eneo hili. Tarehe 20 Mei, 2017, Trump alitembelea Riyadh, na matokeo ya  ziara hiyo pamoja na mambo mengine mengi maovu, ilikuwa ni Saudia kuihonga Marekani dola bilioni 110 kwa madai ya makubaliano ya kijeshi baina ya nchi hizo mbili.

Kwa kweli watawala wanagenzi wa Saudi Arabia wanatoa madai ya uongo dhidi ya wengine ili kuficha siasa zao ovu katika eneo hili. Wanashirikiana na Wamarekani katika vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hilo linaonesha ni kiasi gani viongozi hao wanatumia siasa za kigeni kama wenzo tu wa kufanikishia mambo yao. Ushindani wa kununua silaha unaofanywa na Saudi Arabia unatokana na udhaifu wa nchi hiyo katika eneo la Asia Magharibi na wanadhani kwamba kwa kuzihonga nchi kubwa ili ziwalindie usalama wao, viongozi hao wa Saudi Arabia wanadhani kuwa wataifanya nchi yao kuwa yenye nguvu katika eneo hili. Hata hivyo tajiriba iliyopatikana katika matukio mbalimbali kama vile kupinduliwa vibaraka wakubwa wa Marekani kama Hosni Mubarak wa Misri, ni ushahidi wa wazi wa upofu wa fikra hiyo ya viongozi wa Saudi Arabia. Mwanzoni mwa mwezi huu wa Juni, Amin al Qamuria, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati raia wa Lebanon aliliambia shirika la habari la IRNA kwamba, chimbuko la matatizo mengi ya eneo hili ni kwamba Saudi Arabia inataka kuzifanya nchi zote za eneo hili kuwa watiifu kwake na zifuate kibubusa sisa zake ghalati.

Saudia inatumia silaha inazopewa na nchi za Magharibi kufanya jinai za kuchupa mipaka dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen

 

Ni jambo lililo wazi kwamba, madola ya kibeberu hayako tayari kupoteza fedha nyingi mno yanazozipata kupitia mikataba ya kijeshi na nchi za Kiarabu hususan Saudi Arabia. Mabeberu hao wanatumia mbinu za kila namna ikiwemo kutishia usalama wa tawala hizo za Kiarabu, ili wapate muradi wao. Siasa alizokuja nazo rais wa Marekani, Donald Trump na chama chake cha Republican zilikuwa ni pamoja na kuitishia Saudi Arabia kulipa gharama za mashambulio ya Septemba 11 nchini Marekani kutokana na kuthibiti uchunguzi kwamba magaidi wengi waliofanya mashambulio hayo huko Marekani walikuwa ni raia wa Saudi Arabia. Rais huyo wa Marekani amekuwa akitangaza wazi kuwa, nchi za Kiarabu haziwezi kuwepo bila ya ulinzi wa Marekani, hivyo kwa mtazamo wa Trump, ni wajibu kwa wanasiasa za Marekani kufyonza vilivyo fedha za mafuta za nchi kama Saudi Arabia.