Wanajeshi wa Israel wamewaua Wapalestina watatu Quds Tukufu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i31748-wanajeshi_wa_israel_wamewaua_wapalestina_watatu_quds_tukufu
Wapalestina watatu wamepigwa risasi na kuuawa baada ya kufyatuliwa risasi na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 14, 2017 03:10 UTC
  • Wanajeshi wa Israel wamewaua Wapalestina watatu Quds Tukufu

Wapalestina watatu wamepigwa risasi na kuuawa baada ya kufyatuliwa risasi na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds.

Taarifa zinasema kumejiri ufyatulianaji risasi baina ya wanajeshi Wazayuni na Wapalestina karibu na mlango wa Bab al-Asbat katika Msikiti wa al Aqsa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambapo Wapalestina watatu wameuawa shahidi.

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimekiri kuwa wanajeshi wawili wa utawala huo wameuawa na mwingine kujeruhiwa katika mapigano hayo.

Aidha baada ya kujiri mapigano hayo katika eneo la Msikiti wa Al Aqsa, utawala wa Kizayuni umefunga milango yote ya msikiti huo na Wapalestina hawana ruhusa kuingia hapo.

Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakifyatua risasi katika msikiti wa al Aqsa

Duru za Palestina zinadokeza kuwa, katika tukio hilo, wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel wamemkamata mwanamke moja na watoto watatu Wapalestina katika eneo la Bab al-Asbat.

Oparesheni hiyo ya Palestina ni sehemu ya Intifadah au mwamako wa tatu wa Wapalestina uliopewa jina la Intifadha ya Quds na ulianza Oktoba mwaka 2015 katika Msikiti wa al Aqsa. Intifadha hiyo ilianza kufuatia hujuma dhidi ya msikiti huo ambazo zimekuwa zikitekelezwa mara kwa mara na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni pamoja na walowezi wa Kizayuni. Katika Intifadha hii  hadi sasa Wapalestina zaidi ya 330 wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel huku wengine zaidi ya 24000 wakijeruhiwa.