Lebanon yataka mataifa ya ulimwengu yailazimishe Israel iache uvamizi
Rais Michel Aoun wa Lebanon ametoa wito kwa mataifa ya ulimwengu kuchukua hatua ambazo zinataulazimisha utawala haramu wa Israel ukomeshe hatua zake za kivamizi.
Rais wa Lebanon amesema kuwa, nchi za Kiarabu zinapaswa kuchukua hatua madhubuti ambazo zitaufanya utawala huo ghasibu uache uvamizi wake na wakati huo huo uheshimu sheria za kimataifa.
Katika ujumbe wake kwa Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Rais wa Lebanon amelaani uvamizi wa mara kwa mara wa utawala haramu wa Israel dhidi ya msikiti wa al-Aqswa na kisha kufunga milango ya msikiti huo na hivyo kuwazuia waumini kutekeleza ibada ya Swala na kuongeza kuwa, baada ya kukithirisha vitendo vyake vya kivamizi, hivi sasa Israel inaelekea upande wa kuyahujumu maeneo matakatifu.
Rais wa Lebanon amesisitiza kuwa, hatua na hujuma za utawala ghasibu wa Israel zinalenga kubadilisha muundo wa kijamii na kijiografia wa Baytul Muqaddas.
Ameongeza kuwa, ili kukabiliana na hujuma hizo za Israel kuna haja kwa mataifa ya ulimwengu hususan nchi za Kiarabu na kiislamu kuchukua hatua za maana na madhubuti ambazo zitaufanya utawala huo ghasibu usitishe na kukomesha uvamizi wake huo.
Rais Michel Aoun wa Lebanon aidha ameeleza kuwa, nchi za Kiarabu zinapaswa kuziandikia barua taasisi za kimataifa zikiwemo zinazojihusisha na masuala ya haki za binadamu na kutaka kuchukuliwa hatua dhidi ya utawala huo ghasibu.