Al Abadi: Kukombolewa Mosul ni mwanzo wa kumalizika Daesh
(last modified Mon, 17 Jul 2017 07:22:24 GMT )
Jul 17, 2017 07:22 UTC
  • Al Abadi: Kukombolewa Mosul ni mwanzo wa kumalizika Daesh

Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa kushindwa magaidi katika mji wa Mosul kaskazini mwa nchi hiyo ni mwanzo wa kusambaratika kundi la kitakfiri la Daesh.

Akizungumza na Alster Bert Waziri Mshauri wa Uingereza katika Masuala ya Mashariki ya Kati na Afrika, Haidar al Abadi  ameeleza kuwa ushindi ilioupata Iraq na kukombolewa kikamilifu mji wa Mosul ni mwanzo wa kusambaratika kundi la Daesh katika kushirikiana na wakazi wa maeneo yaliyokombolewa na wanamgambo wenye silaha. Waziri Mkuu wa Iraq ameongeza kuwa serikali ya nchi hiyo hivi sasa inafanya juhudi za kurejesha uthabiti na kukabiliana na changamoto zinazoikabili baada ya kutoa pigo kwa Daesh. 

Katika mazungumzo hayo, Alster Bert Waziri Mshauri wa Uingereza katika Masuala ya Mashariki ya Kati na Afrika amepongeza ushindi uliopatikana huko Mosul na kusisitiza kuwa Uingereza itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya Baghdad katika nyanja mbalimbali, katika suala la kuwarejesha wakimbizi wa Kiiraqi nchini kwao na kuiunga mkono Iraq yenye umoja na amani. 

Wairaqi wakisherehekea kukombolewa kikamilifu mji wa Mosul  

Waziri Mkuu wa Iraq tarehe kumi mwezi huu alitangaza kukombolewa kikamilifu mji wa Mosul kutoka mikononi mwa magaidi wa kitakfiri wa Daesh.