Nchi nne za Kiarabu zashadidisha vikwazo vyao dhidi ya Qatar
(last modified Tue, 25 Jul 2017 14:16:25 GMT )
Jul 25, 2017 14:16 UTC
  • Nchi nne za Kiarabu zashadidisha vikwazo vyao dhidi ya Qatar

Nchi nne za Kiarabu zilizovunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar na kuiwekea vikwazo nchi hiyo ya Kiarabu leo zimetoa orodha mpya ya majina ya taasisi na shakhsia zinaodai kuwa wana mfungamano na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Qatar.

Katika taarifa yao ya pamoja iliyotaja majina ya asasi tisa na shakhsia tisa waliojumuishwa kwenye orodha iliyotangulia, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain na Misri zimedai kuwa shughuli za taasisi na watu hao zina uhusiano wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja na viongozi wa Qatar. Taarifa hiyo ya nchi hizo nne imeongeza kuwa wigo wa shughuli na harakati za makundi yenye misimamo ya kufurutu ada mjini Doha umepanuka zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Waqatari watatu na Mkuwaiti mmoja ambao wametajwa kwenye orodha ya pamoja ya Saudia, Imarati, Bahrain na Misri wamehusika katika ukusanyaji misaada ya fedha ya kulisaidia kundi la Jabhatu-Nusra na makundi mengine ya kigaidi. Aidha Wayemeni watatu, Walibya wawili na asasi sita zinazoendesha shughuli zao nchini Libya zimedaiwa kuwa zinasaidiwa kifedha na viongozi wa Qatar.

Viongozi wa nchi nne za Kiarabu zilizoiwekea Qatar vikwazo

Orodha ya vikwazo iliyotolewa na nchi hizo nne za Kiarabu tarehe 9 ya mwezi uliopita wa Juni ilijumuisha watu 59 na taasisi 12 zinazodaiwa kujihusisha na harakati za kigaidi. 

Ili kuiondolea vikwazo zilivyoiwekea Qatar, nchi hizo nne za Kiarabu zikiongozwa na Saudia zimetoa masharti kadhaa ya kutekelezwa na viongozi wa serikali ya Doha ikiwemo kuondoa kituo cha kijeshi cha Uturuki kilichoko nchini Qatar, kuvunja uhusiano na harakati ya Ikhwanul Muslimin na kuifunga kanali ya televisheni ya Aljazeera, masharti ambayo Qatar imekataa kuyatekeleza.../

Tags