UN: Mzingiro dhidi ya Ghaza unapasa kuhitimishwa
Msemaji wa Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ametaka kuhitimishwa mzingiro wa utawala ghasibu wa Isarel dhidi ya Ukanda wa Ghaza.
Ravina Shamdasani ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza na kueleza kuwa, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, Israel ndiyo inayopaswa kulinda haki za wakazi wa Ukanda wa Ghaza kwa kuwa ndiyo inayolikalia kwa mabavu eneo hilo.
Msemaji wa Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu taathira mbaya na madhara ya kukatwa umeme huko Ghaza na kukosekana huduma za msingi za afya, tiba na maji safi na salama kwa raia wa Kipalestina wa eneo hilo na kusisitiza kuwa, kukatwa mara kwa mara huduma ya umeme kunatishia maisha ya makundi dhaifu ya wakazi eneo hilo lililo chini ya mzingiro wa Israel.
Utawala wa Kizayuni wa Israel unalizingira eneo la Ghaza tangu mwaka 2006 baada ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kuibuka mshindi katika uchaguzi wa Bunge wa Palestina. Utawala huo haramu unazuia kuingizwa madawa na vifaa vya ujenzi katika eneo hilo.