Mar 18, 2016 16:38 UTC
  • Mahmoud Abbas aunga mkono mpango wa 'amani' wa Ufaransa

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesisitiza tena juu ya uungaji mkono wake kwa mpango uliopendekezwa na Ufaransa wa kuitishwa mkutano wa kimataifa kwa ajili ya mazungumzo ya mapatano ya Mashariki ya Kati.

Mahmoud Abbas ametoa msimamo huo katika mazungumzo na Pierre Vimont, mjumbe wa Ufaransa katika masuala ya amani ya Mashariki ya Kati na kueleza kuwa Palestina inakubaliana na mpango wa Ufaransa wa kuitisha mkutano wa kimataifa wa amani na iko tayari kutoa ushirikiano kamili kwa Paris.

Itakumbukwa kuwa mwezi uliopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Lauren Fabius, alitangaza kwamba nchi hiyo inafanya jitihada za kufanikisha kufanyika mkutano wa kimataifa kwa lengo la kutekeleza mpango wa kuunda nchi mbili katika ardhi za Palestina. Fabius alifafanua kuwa endapo jitihada hizo hazitozaa matunda, Ufaransa itaitambua rasmi nchi huru ya Palestina.

Hayo yanajiri katika hali ambayo Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetahadharisha kuwa mpango unaopendekezwa na Ufaransa una madhara kwa wananchi wa Palestina na maslahi yao ya kitaifa na kutangaza kuwa hakika ya mpango huo ni kujaribu kufufua mazungumzo ya mapatano yaliyofeli kati ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala ghasibu wa Kizayuni na kutaka kuizima Intifadha ya kishujaa ya Ufukwe wa Magharibi na Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu.../

Tags