Mji wa Tal Afar Iraq wakombolewa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33656-mji_wa_tal_afar_iraq_wakombolewa
Duru za Iraq zimetangaza kuwa mji wa Tal Afar wa magharibi mwa mkoa wa Nainawa (Nineve) huko kaskazini mwa Iraq umekombolewa siku ya saba tangu ilipoanza operesheni ya kuwafurusha magaidi wa ISIS (Daesh) mjini humo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 26, 2017 11:20 UTC
  • Mji wa Tal Afar Iraq wakombolewa

Duru za Iraq zimetangaza kuwa mji wa Tal Afar wa magharibi mwa mkoa wa Nainawa (Nineve) huko kaskazini mwa Iraq umekombolewa siku ya saba tangu ilipoanza operesheni ya kuwafurusha magaidi wa ISIS (Daesh) mjini humo.

Mwandishi wa Radio Tehran amenukuu taarifa ya kitengo cha habari za kijeshi cha Iraq ikisema kuwa, mji wa Tal Afar umekombolewa kutokana na ushirikiano wa karibu wa vikosi vya kujitolea vya wananchi, taasisi ya kupambana na ugaidi ya Iraq, jeshi na polisi ya shirikisho la nchi hiyo chini ya kivuli cha fatwa na Marjaa wa kidini wa nchi hiyo.

Kabla ya hapo, Abdul Amir Rashid Yarallah, kamanda wa operesheni ya pamoja ya Iraq ya kupambana na ugaidi alikuwa amesema kuwa, vikosi vya nchi hiyo vilikuwa vimeshakomboa asilimia 90 ya mji huo ambao Daesh walikuwa wanauita ni Mosul ndogo.

Jeshi la Iraq likiingia mjini Tal Afar

 

Komandi ya Operesheni za Pamoja ya Iraq imesisitiza kuwa, jukumu la Polisi ya Federali na vikosi vya kujitolea vya wananchi maarufu kwa jina la al Hashd al Shaabi la kuukomboa mji wa Tal Afar limekamilika.

Wakati huo huo Haydar al Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq ambaye ndiye amirijeshi mkuu wa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo ameelekea mjini Tal Afar kwa ajili ya kutangaza rasmi kukombolewa mji huo.

Zoezi la kuukomboa mji wa Tal Afar kutoka mikononi mwa genge la kigaidi la Daesh lilianza rasmi tarehe 20 mwezi huu wa Agosti yaani siku saba zilizopita.