Sep 01, 2017 15:03 UTC
  • Utawala wa Bahrain waendelea kuzuia Sala ya Ijumaa

Vikosi vya usalama nchini Bahrain leo vimewazuia tena Waislamu wa eneo la Diraz kusali Sala ya Ijumaa.

Taarifa zinasema kuwa, vikosi vya usalama vya utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain vimeingia katika eneo la Diraz katika mji mkuu Manama na kuwazuia wakaazi wa eneo hilo kusimamisha Sala ya Ijumaa katika msikiti wa Imam Swadiq AS.  Waumini waliofika hapo walilazimika kusali Sala ya Adhuhuri furada kufuatia mzingiro wa vikosi vya usalama.

Kanali ya televisheni ya Februari 14 ya Bahrain imetangaza kuwa,  Aklhamisi usiku idadi kubwa ya watu waliandamana katika eneo la Diraz kupinga ukandamizaji unaofanywa na vikosi vya usalama.

Mnamo Juni 20, 2016, utawala wa walio wachache wa Aal Khalifa ulimpokonya Ayatullah Sheikh Qassim uraia wake na baada ya hapo kuvunja Taasisi ya Mafundisho ya Kiislamu iliyoasisiwa na mwanazuoni huyo. 

Sheikh Issa Qassim

Tokea wakati huo eneo la Diraz ,ambako yamo makazi ya Sheikh Qassim, limekuwa chini mzingiro mkali wa vikosi vya Bahrain ambavyo vinawakandamiza Waislamu.

Tangu Februari 14 mwaka 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia vuguvugu la mapinduzi ya wananchi dhidi ya utawala kibaraka na wa kidikteta wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanataka kuweko uhuru, uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuingia madarakani serikali ambayo imechaguliwa na wananchi wenyewe. Hatua zote za utawala huo za kuzima vuguvugu hilo hadi sasa hazijafanikiwa.

Tags