Uturuki: Ikiwa Kurdistan itaendelea na kiburi tutaikabili kwa vikwazo na jeshi
Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ametoa onyo kali akisema kuwa, ikiwa viongozi wa eneo la Kurdistan wataendelea na kujichukulia maamuzi ya upande mmoja, basi Ankara italazimika kuliwekea vikwazo eneo hilo sambamba na kutekeleza chaguo la kijeshi.
Rais Tayyip Erdoğan ameyasema hayo leo mjini Istanbul na kuongeza kuwa, machaguo yote dhidi ya eneo la Kurdistan la Iraq kukiwemo kufunga bomba la kusafirishia mafuta eneo la kaskazini mwa Iraq, kufungwa vyanzo vya forodha na hata kijeshi, yote yako mezani. Akibainisha kuwa Uturuki kamwe haitoruhusu kuundwa serikali bandia katika mipaka ya kusini mwa nchi hiyo amesema kuwa, msimamo wa Ankara kuhusiana na suala hilo uko wazi na kwamba inayachukulia matokeo ya kura ya maoni ya kutaka kujitenga eneo hilo kuwa ni bandia.
Amesema kuwa katika kipindi hiki, taifa na watu wa Iraq wanahitajia umoja na mshikamano na hivyo hatua ya viongozi wa eneo la Kurdistan la Iraq ya kutaka kujitenga, haikubaliki kwa namna yoyote ile. Rais Recep Tayyip Erdoğan ameongeza kuwa, Ankara itakabiliana kwa nguvu zake zote na hatua yoyote ambayo itatishia usalama wa mipaka ya Uturuki. Katika siku za hivi karibuni viongozi wa serikali ya Uturuki, Iraq na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara kadhaa wameitaja kura ya maoni ya kutaka kujitenga eneo tajwa kuwa isiyo sahihi sambamba na kuonya juu ya matokeo mabaya ya hatua hiyo katika eneo.
Katika hatua za awali za kukabiliana na kura hiyo ya maoni, Jumapili ya jana Uturuki na Iran zilifunga mipaka yao na eneo hilo sambamba na kuzuia safari zote za anga kuingia na kutoka Kurdistan. Utawala haramu wa Kizayuni wa Irael na Marekani zinatajwa kuwa nyuma ya mpango huo wa kutaka kuligawa vipande taifa la Iraq.