Imarati yaitaka Qatar isiandae Kombe la Dunia 2022
Afisa wa ngazi za juu wa usalama katika Umoja wa Falme za Kiarabu amesema mgogoro uliopo kati ya Doha na nchi kadhaa za Kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia utapatiwa ufumbuzi iwapo Qatar itaachana na azma yake ya kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2022.
Dhahi Khalfan, Mkuu wa Usalama mjini Dubai ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: Iwapo Kombe la Dunia 2022 halitaandaliwa na Qatar, mgogoro wa Qatar utaisha.
Hadi tunaenda mitamboni, serikali ya Qatar ilikuwa haijatoa maelezo kuhusu pendekezo hilo la afisa wa ngazi za juu wa Imarati.
Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri tarehe Tano Juni mwaka huu zilitangaza kukata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar zikiituhumu Doha kuwa inaunga mkono ugaidi na kwamba haiendi sambamba na malengo ya nchi hiyo.
Baada ya kukata uhusiano huo wa kidiplomasia, nchi nne hizo za Kiarabu baadaye ziliiwekea Qatar mzingiro wa kiuchumi na kuipa masharti chungu nzima.
Qatar inakadhibisha madai ya kuunga mkono ugaidi na inasisitiza kuwa, ni nchi inayojitawala na kamwe haitafuata siasa za kiimla za Saudia.