Marekani, Israel na Saudia zinapanga njama ya kuizingira Hizbullah
Gazeti moja la nchini Lebanon la al-Akhbar limeandika kuwa, hivi sasa Marekani, Saudia na Israel zinapanga njama kwa ajili ya kuidhibiti harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ili kuizuia isiweze kutumia uwezo wake katika vita vijavyo vya kuainisha hatima.
Gazeti hilo limeandika kuwa, njama kubwa kwa ajili ya kuiondoa Iraq katika mstari wa muqawama tayari zimeanza na moja ya njama hizo ni kuligawa taifa hilo la Kiarabu na kuasisi utawala wa kikaumu na kikabila sambamba na kuiepusha serikali ya Baghdad na siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa mujibu wa gazeti hilo, hatua ya pili itakayofuatia baada ya njama hizo za Marekani, Saudia na Israel dhidi ya Iraq, ni kusimamisha kabisa miradi eti ya nyuklia ya Iran na kuirudisha nyuma nchi hii kupitia vikwazo na mzingiro zaidi kwa lengo la kuitenga sambamba na kuisukuma kwenye matatizo makubwa ya kiuchumi na vita pamoja na Wakurdi.
Kadhalika gazeti la al-Akhbar la nchini Lebanon limefafanua kuwa, baada ya magaidi wa Syria kushindwa na jeshi la nchi hiyo, sasa Washington inajitahidi kuwachochea Wakurdi kusimama dhidi ya serikali ya Damascus sambamba na kuwashawishi watu wa jamii hiyo waweze kujitenga na serikali. Katika uwanja huo, gazeti hilo limefafanua kuwa Rais Donald Trump wa Marekani anajiandaa kupitisha sheria itakayoiwekea harakati hiyo ya Hizbullah vikwazo zaidi.