Onyo la Syria kwa utawala haramu wa Israel
Jeshi la Syria limeuonya utawala haramu wa Israel kuhusiana na kukariri uvamizi wake dhidi ya ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Jumatatu ya juzi tarehe 16 Oktoba, jeshi la Syria lilisisitiza kwamba, litaendelea na mapambano na vita vyake dhidi ya magaidi. Kabla ya hapo, duru za utawala ghasibu wa Israel zilikuwa zimetangaza kuwa, juzi Jumatatu, kikosi cha anga cha Israel kiliushambulia mfumo wa makombora ya kutungulia ndege wa Syria jirani na mji mkuu Damascus. Aidha kabla ya hapo pia, Israel ilikuwa imevurumisha makombora kadhaa dhidi ya mkoa wa Rif Dimashq kusini mwa Syria.
Katika miaka ya hivi karibuni na kufuatia kuibuka mgogoro wa Syria, utawala wa Kizayuni wa Israel, mara kadhaa umefanya mashambulio ya anga dhidi ya ngome za jeshi la Syria katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo kwa shabaha ya kuwaunga mkono magaidi. Utawala wa Kizayuni wa Israel na madola ya Magharibi yakitumia vibaya malalamiko ya baadhi ya makundi dhidi ya serikali ya Syria, yamekuwa yakitoa misaada ya kilojistiki kwa magaidi na waendesha machafuko na hivyo kuzidi kuitumbukiza nchi hiyo katika vurugu na machafuko.
Kwa hakika utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa na nafasi kubwa katika mgogoro wa Syria kutokana na kuyaunga kwake mkono makundi ya kigaidi na kitakfiri. Israel imetumia vibaya mazingira ya sasa ya Syria na kuchochea mgogoro wa nchi hiyo.
Utawala huo vamizi unataka kushadidisha harakati zake za kijeshi dhidi ya Syria ili iandae uwanja wa kuendelea kushuhudiwa harakati za magaidi katika maeneo muhimu na ya kiistratejia ya nchi hiyo ya Kiarabu. Aidha mashambulio ya Israel huko nchini Syria yanabainisha ukweli mwingine nao ni uchu na tamaa ilionao utawala huo wenye kupenda kujitanua katika ardhi ya Syria.
Utawala ghasibu wa Israel ambao mwaka 1967 ukiendeleza siasa zake za kujitanua katika eneo na Mashariki ya Kati uliikalia kwa mabavu miinuko ya Golan ya Syria, umekuwa ukitumia njia mbalimbali ili kuimarisha uvamizi wake huo huko Syria.
Fauka ya hayo na katika fremu ya mikakati yake ya kutaka kutekeleza ndoto yake ya kuunda dola kubwa la Israel kuanzia Mto Nile mpaka Furati na vile vile kufanya harakati katika njia ya kutekeleza mipango yenye njama ya Magharibi katika eneo hili, utawala huo ghasibu umekuwa ukifuatilia mipango yake ya kujitanua katika Mashariki ya Kati na kuhuisha mipango kama ule wa Mashariki ya Kati Kubwa au Mashariki ya Kati Mpya.
Moja ya misingi mikuu ya mipango ya Israel na Marekani ni kuzigawa zaidi nchi za Mashariki ya Kati na kutumia wenzo wa kijeshi kwa ajili ya kuzusha hofu na wahaka na hivyo kusukuma mbele malengo yao. Kwa mujibu wa mipango iliyotangazwa kuhusiana na mpango unaojulikana kama Mashariki ya Kati Kubwa, nchi za Iraq na Syria ni miongoni mwa nchi zulizoko katika mpango huo.
Hata hivyo kusimama kidete kunakofaa kupigiwa mfano kwa jeshi na wananchi wa Syria na Iraq mbele ya magaidi, kivitendo kumevuruga kabisa mahesabu yote ya Israel na Marekani katika Mashariki ya Kati, ambapo hivi sasa siku za kushindwa na kusambaratishwa kikamilifu magaidi hao zinahesabika.
Hii ni katika hali ambayo, viongozi wa Syria sambamba na kusisitiza juu ya udharura wa kuhitimishwa uvamizi na ukaliaji mabavu wa Israel, wametahadharisha pia kuhusiana na ukiukaji wa anga ya nchi hiyo unaofanywa mara kwa mara na Tel Aviv. Kwa hakika, misimamo ya Syria kuhusiana na uvamizi wa Israel, inabainisha kushindwa njama zote za kuipotosha Damascus na kuifanya iache kuzingatia hatua na harakati za utawala huo vamizi.
Wananchi na jeshi la Syria wako macho ambapo sambamba na kufuatilia kwa karibu nyendo za kivamizi za utawala wa Israel, wamejiandaa kikamilifu kutoa jibu mwafaka kwa utawala huo ghasibu.
Onyo na indhari za mara kwa mara za Syria kwa Israel ni kengele ya hatari kwa utawala huo wenye kupenda vita na ishara ya kuizindua jamii ya kimataifa ambayo imenyamazia kimya uvamizi wa Israel katika eneo nyeti la Mashariki ya Kati.