Tishio la Wamarekani kuanzisha machafuko mapya Asia Magharibi
Maafisa wawili wa ngazi za juu kiusalama nchini Mrekani wamefichua mipango mipya ya serikali ya nchi hiyo ya kuzua vurugu na machafuko katika eneo la Asia Magharibi.
Wakizungumzia suala hilo hivi karibuni, Mike Pompeo, Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA na Jenerali Herbert Raymond McMaster, Mashauri wa Usalama wa Kitaifa wa Rais Donald Trump wa Marekani, wameituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni tishio la kushughulikiwa haraka katika eneo la Mashariki ya Kati na kusisitiza kubuniwa muungano wa kieneo na kimataifa kwa ajili ya kukabiliana nayo. Huku wakikariri ukosoaji wao wa mapatano ya nyuklia kati ya Iran na nchi sita muhimu za dunia, yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA, maafisa wawili hao wa Marekani wamesema kuwa Washington itakabiliana na nafasi ya kieneo ya Iran pamoja na nguvu yake ya kiulinzi.
Matamshi hayo yanatolewa katika hali ambayo kutokana na kushindwa mara kwa mara kwa kundi la kigaidi la Daesh, ineoonekana kuwa eneo la Asia Magharibi linakaribia kushuhudia utulivu wa kiwango fulani baada ya kushuhudia miongo miwili ya vita vya umwagaji damu vilivyochochewa na Marekani pamoja na washirika wake katika eneo. Sehemu kubwa ya amani na utulivu huo inatokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kukabiliana na makundi ya kigaidi kama vile Daesh yanayodhaminiwa na kupewa misaada ya kijeshi na kifedha na muungano wa nchi za Magharibi na Kiarabu. Muungano huo unaoongozwa na Marekani una wasiwasi kwamba iwapo Daesh itaangamizwa, eneo hili kama unavyodai, litadhibitiwa na Iran. Hii ni katika hali ambayo uzoefu wa miaka 20 iliyopita nchini Afghanistan, Iraq na Syria unathibitisha wazi kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikipambana vikali dhidi ya makundi ya kigaidi katika nchi hizo, na kuwa tayari kushirikiana na pande zote husika kwa ajili ya kuleta uthabiti na utulivu katika eneo hili.
Pamoja na hayo, Marekani imeonyesha mara tu baada ya kunufaika na msaada wa Jamahuri ya Kiislamu ya Iran katika kutatua matatizo ya kiusalama katika eneo, huigeukia ghafla na kuielekezea kidole cha lawama kuwa ndiyo inayochochea machafuko na ghasia katika eneo hili. Hali hiyo ilionekana wazi baada ya kufanyika mazungumzo ya mjini Bonn na Maghdad kwa ajili ya kutatua matatizo ya kiusalama baada ya utawala wa Taliban nchini Afghanistan na wa dikteta Saddam huko Iraq, na sasa hali hiyo inaonekana kukaririwa na serikali ya Marekani baada ya kukaribia kuangamizwa magaidi wa Daesh.
Pamoja na hali hiyo, Nafasi ya Iran katika eneo la Asia Magharibi haifungamani kwa vyovyote vile na matakwa ya Marekani na washirika wake. Kwa maneno mengine ni kuwa ushaiwshi wa Iran katika eneo hili unatokana moja kwa moja na uwezo wa kitaifa, kutolewa mifano bora na kukatishwa tamaa mataifa ya eneo kuhusiana na uvunjaji ahadi wa mara kwa mara wa nchi za Magharibi.
Kwa msingi huo ushawishi huo wa Iran unaoongezeka siku baada ya nyingine hauwezi kufutwa kwa vitisho na utiaji hofu, hata kama jambo hilo linaweza kuanzisha duru nyingine ya machafuko, ghasia na mivutano ya umwagaji damu katika eneo.
Kwa mtazamo wa Marekani na washirika wake wa kieneo ukiwemo utawala haramu wa Israel na vilevile Saudi Arabia, utulivu na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi unakinzana na maslahi yao ya kitaifa na kwa msingi huo, nchi hizo zinatumia kila njia ili kuyaweka mataifa ya eneo hili katika hali ya machafuko, vita na mauaji. Hivi sasa pia zamu imefika kwa ajili ya nafasi chanya ya kieneo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, shughuli za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH na uwezo wa makombora wa Iran kutiliwa shaka na kupigiwa ngoma ya vitisho na nchi hizo.