WFP latahadharisha kuhusiana na uhaba wa chakula nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i3661-wfp_latahadharisha_kuhusiana_na_uhaba_wa_chakula_nchini_yemen
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limetahadharisha kuhusiana na uhaba mkubwa wa chakula unaoikabili nchi ya Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 23, 2016 21:23 UTC
  • WFP latahadharisha kuhusiana na uhaba wa chakula nchini Yemen

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limetahadharisha kuhusiana na uhaba mkubwa wa chakula unaoikabili nchi ya Yemen.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limetangaza kuwa, takribani nusu ya mikoa yote 22 ya Yemen inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na vita na kwamba, mikoa hiyo inaelekea kukumbwa na ukame.

Taarifa hiyo ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP imeeleza kuwa, zaidi ya raia milioni 13 wa nchi hiyo wanahitajia msaada wa chakula.

Adham Muslim, Naibu Mkurugenzi wa Ofisi ya Mpango wa Chakula Duniani katika mji mkuu wa Yemen Sana'a amesema kuhusu usalama wa chakula, kwamba mikoa 10 kati ya 22 ya nchi hiyo imo katika hali ya hatari na inakaribia kukumbwa na ukame.

Afisa huyo wa WFP katika mji wa Sana'a amebainisha kuwa, vita vya mwaka mmoja nchini Yemen vimewafanya raia milioni mbili na laki tatu kuwa wakimbizi huku zaidi ya nusu ya wakazi milioni 26 wa nchi hiyo wakihitajia msaada wa chakula.

Tangu mwezi Machi mwaka 2015 hadi sasa Saudi Arabia imeiwekea mzingiro wa angani na baharini Yemen na kuzuia misaada ya kibinadamu isiwafikie wananchi wa nchi hiyo, lengo likiwa ni kuiondoa madarakani harakati ya wananchi ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake Abdu Rabbuh Mansour Hadi. Mashambulio ya Saudia dhidi ya Yemen yameangamiza na kusababisha hasara kubwa pia kwa miundombinu ya nchi hiyo, mbali na kulenga na kubomoa hospitali, shule, nyumba za raia na misikiti nchini humo.