Waziri wa zamani wa Israel ajifakharisha kwa mauaji dhidi ya Wapalestina
Waziri wa zamani wa vita wa utawala haramu wa Israel amejifakharisha kwa mauaji aliyoyafanya dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.
Moshe Ya'alon amesema kwa fakhari kubwa kwamba, yeye ndiye aliyewaua zaidi Wapalestina na Waarabu kuliko kiongozi na afisa mwingine yeyote yule wa Israel. Katika hali ambayo, nchi za Kiarabu kama Imarati na Saudi Arabia zinafanya kila ziwezalo kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel, Moshe Ya'alon, waziri wa zamani wa vita wa utawala huo ghasibu amesema hadharani tena kwa kujifakharisha kabisa katika kongamano katika mji wa Herzliya huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) kama ninavyomnukuu:
"Hakuna mtu yeyote si katika Bunge la Israel Knesset na wala katika Baraza la Mawaziri ambaye alikuwa na nafasi kubwa ya kuuawa Wapalestina kama mimi."
Aidha Moshe Ya'alon, amemtaka Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel ajiuzulu kutokana na kukabiliwa na tuhuma za ufisadi na kuongeza kuwa, Netanyahu amekuwa akifanya juhudi za kubakia katika wadhifa wake kwa ajili ya maslahi yake binafsi.
Wakati huo huo, mamia ya Wazayuni wameandamana tena mashariki mwa mji wa Tel Aviv wakitoa wito wa kuharakishwa mchakato wa uchunguzi na usaili dhidi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.