Askari wa Kizayuni wamewakamata Wapalestina 450 mwezi Novemba
Kituo cha Utafiti wa Wafungwa Wapalestina PPCS kimetangaza kuwa jumla ya Wapalestina 450 walikamatwa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel mwezi uliopita wa Novemba.
Msemaja wa PPCS Riyadh al-Ashqar amesema watoto 80 na wanawake 22 ni kati ya Wapalestina ambao walikamatwa kidhulma na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Aidha amesema 150 kati ya wafungwa hao walikamatwa katika eneo la mji wa al-Quds.
Ashqar amesisitiza kuwa, idadi ya Wapalestina waliofungwa maisha iliongezeka Novemba na kufika watu 509.
Hivi sasa kuna Wapalestina 6,280 wanaoshikiliwa katika jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel ambapo wanakabiliwa na mateso makubwa huku wengi wao wakiwa wanashikiliwa kwa muda mrefu pasi na kufunguliwa mashtaka.
Itakumbukwa kuwa jumla ya wafungwa 1,600 wa Kipalestina wanaoshikiliwa na utawala ghasibu wa Israel, walianzisha mgomo wa kula chakula tangu tarehe 17 Aprili na kuendelea kwa takribani siku 40, katika kulalamikia miamala mibaya na kukanyagwa haki zao za kimsingi katika jela za Israel.
Mgomo huo uliongozwa na Marwan Al-Barghuthi kwa kaulimbiu ya "Uhuru na Heshima" katika magereza yote ya utawala wa Kizayuni.