Dec 27, 2017 13:57 UTC
  • Kongamano la Quds, Mji Mkuu wa daima wa Palestina

Viongozi wa kisiasa wa Palestina wametangaza kuwa, Intifadha ya Wapalestina itaendelea hadi pale rais wa Marekani atakapobatilisha uamuzi wake wa kuitambua Quds Tukufu kama mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wameyatamka hayo Jumanne katika 'Kongamano la Quds, Mji Mkuu Daima wa Palestina' ambalo limeandaliwa na Harakati ya Jihad Islami. Washiriki wa kikao hicho wametaka kuhuishwa umoja wa kitaifa, kushirikishwa Wapalestina wote katika siasa na kuundwa  jeshi la kitaifa kwa ajili ya kulinda matukufu ya ardhi ya Palestina.

Matukio ya Palestina yanaonyesha kuendelea Intifadha hadi wakati wa kutimuliwa Wazayuni kutoka katika ardhi za Palestina. Aidha Wapalestina wamewasilisha ramani ya njia ya kukabiliana na njama za Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Palestina.

Itakumbukwa kuwa tarehe Sita Disemba mwaka huu Rais Donald Trump wa Marekani alitangza Quds Tukufu kuwa eti ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni na kutangaza kuwa atauhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Quds.

Njama za Marekani ni sehemu ya mpango mkubwa wa nchi hiyo kwa lengo la kubadilisha utambulisho wa eneo la Asia Magharibi au Mashariki ya Kati na kulipa eneo hilo utambulisho wa Kizayuni na hivyo kuufanya utawala wa Kizayuni unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu kuwa kitovu cha Mashariki ya Kati iitakayo Marekani.

Katika fremu ya njama hii ndio utawala haramu wa Israel unatekeleza mpango unaojulikana kama 'Quds Kubwa' unaojumuisha kueneza vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi na kulazimisha Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi kutekeleza sera za Israel. Lengo kuu la njama hizo ni kufuta kabisa kadhia na utambulisho wa Palestina.

Ismail Haniya

Katika radiamali yake kuhusu njama hizi, Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amesisitiza kuwa: "Mji wa Quds ulioungana ni mji mkuu wa nchi huru ya Palestina na nchi za Kiarabu na Kiislamu hazitafumbia macho Quds Tukufu."

Ismail Haniya ameongeza kuwa: "Quds ni mji mkuu wa kisiasa wa Palestina, ni mji mkuu wa Waislamu wote duniani na pia Quds ni mji mkuu wa wanadamu, akhlaqi na thamani kwa wapenda uhuru kote duniani wawe ni Waislamu au Wakristo. Quds ni ya Wapalestina wote hivyo watu wa Palestina hawatalegeza kamba hata kidogo kuhusu haki hii."

Tukiangazia sehemu muhimu ya malengo ya njama za Marekani kuhusu Palestina, inatubainikia wazi kuwa, kuna daraja kadhaa za mipango hatari dhidi ya Palestina.

Hivi sasa katika utawala wa Trump, wakuu wa Marekani wanataka kumaliza kadhia ya Palestina kwa maslahi ya utawala haramu wa Israel. Mkabala  wa njama hiyo ya Marekani, Wapalestina nao pia wanafanya mkakati wa kuimarisha uwezo wao kwa lengo la kuzikomboa ardhi zote za Palestina kutoka katika makucha ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Intifadha ya hivi sasa ambayo ni ya tatu imeenea katika ardhi zote za Palestina hasa katika Ukingo wa Magharibi na inafuatilia lengo hilo la ukombozi kamili wa Palestina. Intifadha hii ya Tatu ina sifa moja ya kipekee nayo ni kufuatilia lengo la kukomboa ardhi zote za Palestina.

Tukiangazia Intifadha hii ya tatu tutaona kuwa ina uwezo wa kufikia lengo la kukomboa ardhi za Palestina na hatimaye kuunda nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Quds Tukufu. Kuleta umoja miongoni mwa makundi mbali mbali ya Wapalestina katika kukabiliana na njama za Israel ni nukta muhimu ambayo mkaundi yote ya Palestina yanapaswa kuzingatia katika harakati za ukombozi.  Umoja utawawezesha Wapalestina kuunganisha nguvu zao ili kushughulikia lengo lao la kuunda nchi huru mji mkuu wa ke ukiwa ni Baytul Muqaddas.

Rais Trump wa Marekani

Intifadha hii ya tatu pia imelipatia umuhimu mkubwa suala la ukombozi wa Quds Tukufu na nukta chanya hapa ni kuwa, lengo hili limepata uungaji mkono mkubwa wa kimataifa na limewatia wasi wasi mkubwa wakuu wa Marekani na utawala wa Kizayuni na ndio sababu Marekani ikatumia lugha ya vitisho kwa nchi zinaounga mkono Palestina.

Sifa nyingine ya Intifadha ya Palestina ni kuungana mkono kwake na mrengo wa Muqawama au mapambano katika eneo hili, jambo ambalo litawawezesha Wapalestina kutumia uwezo mkubwa wa wananchi katika eneo hili katika kupambana kwa mafanikio na njama za Marekani na utawala wa Kizayuni katika masuala mbali mbali hasa kadhia ya Palestina.

Tags