Kufanyiwa mabadiliko muundo wa jeshi la Jordan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i38243-kufanyiwa_mabadiliko_muundo_wa_jeshi_la_jordan
Mfalme Abdallahwa wa Pili wa Jordan amewastaafisha cheo cha ukamanda wa jeshi kaka zake wawili na binamu yake katika hatua ya aina yake kuwahi kuchukuliwa nchini humo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Dec 29, 2017 04:14 UTC
  • Kufanyiwa mabadiliko muundo wa jeshi la Jordan

Mfalme Abdallahwa wa Pili wa Jordan amewastaafisha cheo cha ukamanda wa jeshi kaka zake wawili na binamu yake katika hatua ya aina yake kuwahi kuchukuliwa nchini humo.

Jeshi lina nafasi muhimu katika nchi za Kiarabu za eneo la Mashariki ya Kati; na nafasi ya kamanda wa jeshi pia ina nafasi muhimu katika muundo wa kisiasa na kiusalama wa nchi hizo. Jeshi katika aghalabu ya nchi hizo pia lina nafasi kuu katika upande wa kiuchumi. Jeshi aidha linachangia sehemu muhimu ya vyanzo vya kiuchumi na Jordan ni miongoni mwa nchi hizo.  

Mfalme Abdallah wa Pili wa Jordan ambaye ni mwanajeshi akiwa amesomea masuala ya jeshi huko Marekani na Uingereza anatoa kipaumbele na zingatio kwa suala la kuliimarisha jeshi la nchi hiyo. Mfalme huyo amekuwa akizingatia kufanya mabadliko katika muundo wa vikosi vya ulinzi vya nchi yake tangu mwishoni mwa mwaka jana. Mfalme wa Jordan kabla ya hapo alikuwa ameufanyia mabadliko muundo wa idara za usalama na vikosi vya polisi; na hivi sasa ametoa kipaumbele kulifanyia marekebisho jeshi la nchi hiyo. Ametaja sababu kuu zilizopelekea kufanyiwa mabadiliko muundo wa jeshi la Jordan kuwa ni kushindwa jeshi hilo kupambana na ugaidi, gharama kubwa za kiuchumi na uundaji upya wa mfumo wa jeshi hilo.  

Wanajeshi wa Jordan katika mapambano dhidi ya ugaidi  

Hata kama Jordan katika miaka ya hivi karibuni imekabiliwa na vitisho vichache vya ugaidi ikilinganishwa na nchi nyingine za Kiarabu lakini kuendelea vitisho hivyo kunatoa udharura wa kulijengea uwezo jeshi  la nchi hiyo kwa kubadilishwa muundo wake.

Gharama za kiuchumi ni moja ya sababu kuu zilizomfanya Mfalme Abdallah wa Pili wa Jordan alifanyie mabadiliko jeshi la nchi hiyo. Jordan ambayo kwa upande wa uchumi inahitajia misaada kutoka Saudi Arabia na Marekani hivi sasa inazidi kulemewa na matatizo ya kiuchumi kutokana na kuathirika na siasa za kieneo za Saudia ikiwemo uuungaji mkono wa nchi hiyo kwa ugaidi huko Syria na mvutano baina  ya Riyadh na Qatar. Kwa mfano, hatua ya Saudia, Imarati na Bahrain ya kuizingira Qatar katika muda wa siku 20 za mwanzoni za mzingiro huo pekee ilisababisha hasara ya karibu dola milioni mbili kwa uchumi wa Jordan.

Uungaji mkono wa jeshi la Marekani kwa magaidi huko Syria 

Hii ni kwa sababu mzingiro huo umesababisha kusitishwa uuzaji bidhaa za Jordan kwa Qatar. Kuongezeka matatizo hayo ya kiuchumi ya Jordan kumempelekea Mfalme Abdallah wa Pili wa nchi hiyo kuliweka katika ajenda yake ya kazi suala la kuwastaafisha viongozi wa ngazi ya juu jeshini lengo likiwa ni kupunguza gharama za kijeshi. Mfalme Abdallah wa Pili ameanza kutekeleza mageuzi na kuwaachisha kazi makamanda wa ngazi ya juu jeshini kwa kuanzia na watu wake wa karibu ili kuzuia malalamiko ya maafisa wa jeshi wasio na mfungamano na utawala ulioko madarakani khususan wale wenye mfungamano na koo zenye ushawishi.  

Mfalme Abdallah wa Pili wa Jordan amelazimika kulihuisha upya jeshi la nchi ili kuleta mabadiliko mapya ndani ya jeshi hilo. Ni wazi kuwa mabadliko hayo licha ya kuwa yatapunguza gharama za kijeshi yatalijenga upya jeshi kwa kuwa na makamanda vijana.