Dec 31, 2017 14:47 UTC
  • Waisraeli waandamana dhidi ya Netanyahu kwa wiki ya tano

Maelfu ya Waisraeli wamemiminika mabarabarani kwa wiki ya tano mfululizo kushiriki maandamano ya kushinikiza kufungwa jela Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu kutokana na kashfa za ufisadi wa kifedha zinazomuandama.

Maandamano hayo ya jana usiku katika mji wa Tel Aviv yalifanyika chini ya kaulimbiu "Maandamano ya Fedheha".

Waandamanaji hao wamesikika wakipiga nara zinazosema "Bibi (Netanyahu) nenda nyumbani!", "Fedheha", "Netanyahu apelekwe jela". Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji hao yalikuwa na jumbe zinazosema: Waziri wa Jinai, Msaliti, na Netayahu kupe.

Maandamano ya kutaka kumuondoa madarakani Netanyahu na kuharakishwa uchunguzi dhidi yake yalianza miezi kadhaa iliyopita mjini Tel Aviv na katika maeneo mengine ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Maandamano dhidi ya Netanyahu Tel Aviv

Uchunguzi kuhusu tuhuma za ufisadi na kupokea rushwa ya mamilioni ya dola kutoka kampuni moja ya Ujerumani zinazomkabili Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni ulianza tangu Januari Pili mwaka huu 2017.

Kesi ya msingi inayomkabili Netanyahu inahusiana na kupokea kiasi cha dola milioni moja kutoka kwa Arnaud Mimran, fisadi wa uchumi, raia wa Ufaransa ambazo inasemekana kuwa zilitumika katika kumpigia kampeni Netanyahu.  

Mbali na Tel Aviv, maandamano dhidi ya Netanyahu yamekuwa yakishuhudiwa katika miji ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu kama vile Quds Tukufu, Haifa na Afula.

Tags