Olmert: Tulishindwa na Hizbullah katika vita; ufisadi wa Netanyahu hautasawariki
Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel amekiri kwamba jeshi la utawala huo dhalimu lilishindwa na Hizbullah ya Lebanon katika vita vya mwaka 2006.
Gazeti la al Ra'y al Yaum limemnukuu Ehud Olmert akisema hayo katika kitabu cha maisha yake na kukiri rasmi, waziwazi na kwa ushahidi kamili jinsi jeshi la utawala wa Kizayuni lilivyoshindwa vibaya katika vita lilivyovianzisha mwaka 2006 dhidi ya Lebanon.
Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth limenukuu sehemu ndogo ya maelezo yaliyomo kwenye kitabu hicho cha maisha ya Ehud Olmert na kufichua namna jeshi la utawala wa Kizayuni lilivyoshindwa vibaya kwenye vita hivyo. Limemnukuu Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Israel akisema: "Mimi nakubali kubeba lawama zote za kushindwa katika vita vya pili vya Lebanon."
Olmert aidha amesema, Israel ilishindwa sehemu nyingi na Hizbullah katika vita hivyo vya siku 33 vya mwaka 2006.
Katika kitabu hicho pia, Waziri Mkuu wa zamani wa Israel amelalamika kuwa, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa hivi sasa wa utawala wa Kizayuni na viongozi wengine wengi wa kisiasa wa mrengo wake walifanya njama nyingi za kumuangusha kisiasa.
Pia amemlaumu vikali Netanyahu kwa ufisadi wa kuchupa mipaka usiotasawarika na kusema kuwa, maisha ya Netanyahu na familia yake yamejaa ghururi na kiburi pamoja na ubadhirufu wa kupindukia wa mali ya umma.