UN: Asilimia 72 ya wakazi wa Ghaza hawana usalama wa chakula
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa huko Palestina (OCHA) imetangaza kuwa asilimia 72 ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza hawana usalama wa chakula.
Ocha imeashirika hali ya eneo la Ukanda wa Ghaza na kueleza kuwa, kuzingirwa eneo la Ghaza na utawala wa Kizayuni tangu mwaka 2006 hadi sasa ni kinyume cha sheria na ni kitendo kinachokinzana na sheria na mikataba ya kimataifa na kwamba hatua hiyo imekuwa na athari na madhara makubwa ya kiuchumi na kibinadamu.
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa huko Palestina (OCHA) imeongeza kuwa, ripoti zinaonesha kuwa, uzalishaji wa ndani huko Ghaza umepungua kwa asilimia 50 na kiwango cha watu wasio na ajira kimefikia asilimia 45; kiwango ambacho kimetajwa kuwa cha juu zaidi duniani. Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imeendelea kubainisha kuwa, karibu asilimia 80 ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza wanategemea misaada kutoka nje na sehemu kubwa ya misaada hiyo ni bidhaa za chakula. Vilevile asilimia 40 wa wakazi wa Ghaza wanaishi chini ya mstari wa umaskini.