Utoaji vitisho tena wa Uturuki dhidi ya Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i42422-utoaji_vitisho_tena_wa_uturuki_dhidi_ya_iraq
Baraza la Usalama wa Taifa la Uturuki limetoa taarifa likitishia kwamba ikiwa serikali ya Iraq haitokomesha harakati za chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK) ndani ya ardhi ya nchi hiyo, Uturuki itapeleka tena vikosi vya jeshi lake eneo la kaskazini mwa Iraq.
(last modified 2026-05-13T18:57:29+00:00 )
Mar 30, 2018 22:15 UTC
  • Utoaji vitisho tena wa Uturuki dhidi ya Iraq

Baraza la Usalama wa Taifa la Uturuki limetoa taarifa likitishia kwamba ikiwa serikali ya Iraq haitokomesha harakati za chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK) ndani ya ardhi ya nchi hiyo, Uturuki itapeleka tena vikosi vya jeshi lake eneo la kaskazini mwa Iraq.

Taarifa hiyo aidha imeeleza kuwa: serikali ya Uturuki inatumai kwamba serikali ya Iraq itahitimisha hatua zinazochukuliwa na PKK kaskazini mwa nchi hiyo hususan katika maeneo ya Sanjar na Qandil.

Katika kipindi cha miaka michache iliyopita Uturuki imeshawahi mara kadhaa kutoa vitisho vya kuivamia kijeshi ardhi ya Iraq. Lakini ukweli ni kwamba hatua za aina hiyo hazitoi taswira ya urafiki baina ya nchi jirani, na badala yake hupanda mbegu za chuki na uadui. Kwa kutumia kisingizio cha harakati za wapiganaji wa chama cha PKK ndani ya ardhi ya Iraq au Syria, Uturuki imevamia ardhi za nchi hizo mbili ambazo zina hali tete ya usalama na kuzitia hasara kadhaa.

Wapiganaji wa PKK

Tangu Januari 20 mwaka huu, jeshi la Uturuki limeingia kwenye mji wa Afrin kaskazini mwa Syria na hivyo kuivamia na kuikalia tena kwa mabavu sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Kabla ya hapo pia, yaani tarehe 24 Agosti mwaka 2016, jeshi la Uturuki lilivamia na kuyakalia maeneo mengi ya ardhi ya Syria. Mbali na kupingwa vikali na serikali yenyewe ya Syria, kitendo hicho cha serikali ya Ankara kimelalamikiwa na kukosolewa pia ndani ya Uturuki kwenyewe, kieneo na kimataifa. Serikali halali ya Syria imetangaza mara kadhaa upinzani wake kwa hatua ya Uturuki ya kuvamia maeneo ya ardhi ya nchi hiyo. Mbali na kulaani vikali, serikali ya Damascus imeeleza bayana kwamba mashambulio ya jeshi la Uturuki katika eneo la Afrin ni uchokozi na uvamizi wa wazi dhidi ya ardhi ya Syria. Lakini mbali na serikali ya Syria, wananchi wengi wa Uturuki pamoja na vyama kadhaa vya siasa vikiwemo vinavyoiunga mkono na vinavyoipinga serikali na hata nchi za eneo pia zimepinga operesheni za kijeshi za jeshi la Uturuki ndani ya ardhi ya Syria. Lakini licha ya upinzani wote huo, serikali ya Ankara inasisitiza kuwa itapanua zaidi operesheni zake za kijeshi ndani ya ardhi ya Syria.

Kifaru cha jeshi la Uturuki katika eneo la Afrin, nchini Syria

Vyama vya upinzani nchini Uturuki na hata baadhi ya vile vinavyoiunga mkono serikali, navyo pia vimekosoa operesheni za kijeshi zinazofanywa ndani ya ardhi ya Syria. Kwa mfano kiongozi wa chama chenye mielekeo ya Kiislamu cha Saadat, Temel Karamollaoğlu, hivi karibuni alitoa tamko la kulaani uingiliaji unaofanywa na serikali ya nchi hiyo katika masuala ya ndani ya Iraq na Syria na uungaji mkono wake kwa baadhi ya makundi ya kigaidi kwa kutoa indhari kwamba: “Serikali ya Ankara itapaswa kuubeba mzigo wa madhara yatakayotokana na uvamizi wake Syria na Iraq”.

Temel Karamollaoğlu

Naye Kemal Kılıçdaroğlu, kiongozi wa chama cha Wananchi cha Jamhuri (CHP) amebainisha kinachoendelea nyuma ya pazia la uvamizi wa kijeshi unaofanywa na serikali ya nchi hiyo kwa kusema: “Serikali ya Uturuki inataka kuipindua serikali halali ya Bashar al-Assad, lakini hadi sasa jambo hilo halijaweza kutokea; na Erdogan hajapata chochote kwa kutoa ahadi za kufanikisha jambo hilo isipokuwa kuchafua sura ya serikali yake katika eneo na duniani kwa jumla”.

Mbali na hasara inazozisababishia Iraq na Syria, hujuma na mashambulio ya kijeshi ya Uturuki yametoa mwanya na fursa kwa makundi yenye misimamo ya kufurutu mpaka ndani ya nchi hizo mbili kuitumia vibaya hali hiyo ili kuweka kambi zao za kijeshi na hata kuvutia wanachama wapya ndani ya nchi hizo…/