Mar 31, 2018 03:59 UTC
  • Rais Erdoğan: Tunajiandaa kuanzisha operesheni kubwa ya kijeshi kaskazini mwa Syria

Licha ya serikali ya Syria kupinga uvamizi wa jeshi la Uturuki katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo, kwa mara nyingine Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ametangaza kwamba jeshi la nchi yake linajiandaa kuanzisha operesheni mpya katika eneo hilo.

Erdoğan alisema hayo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, lengo la operesheni hiyo mpya kaskazini mwa Syria ni kuwaondoa Wakurdi wenye silaha katika maeneo ya Kobanî, Ras al-Ayn na Tell Abyad. Kadhalika Erdoğan amemkosoa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ambaye ametoa pendekezo la kuwa mpatanishi kati ya Ankara na chama cha Kikurdi cha Partiya Yekîtiya Demokrat PYD na kusema kuwa, ni jambo la kusikitisha kuona kwamba Paris inafuata siasa ghalati kuhusiana na mgogoro wa Syria.

Uvamizi wa jeshi la Uturuki kaskazini mwa Syria

Wakati huo huo, Ibrahim Kalin, Msemaji wa Rais wa Uturuki ametupilia mbali upatanishi wowote au mazungumzo na makundi ya Kikurdi kufuatia pendekezo la Ufaransa na kusema kuwa, kuna udharura wa kuchukuliwa hatua kali dhidi ya makundi ya kigaidi badala ya kulegeza kamba na kuyapa uhuru makundi hayo. Jeshi la Uturuki lilianzisha operesheni zake tarehe 20 Januari mwaka huu katika mji wa Afrin, kaskazini mwa Syria kwa kile kilichodaiwa na Ankara kwamba ni kupambana na makundi ya kigaidi ya PKK na PYD, chini ya upinzani mkali wa serikali ya Syria na baadhi ya nchi za eneo.

Jeshi la Uturuki limeshirikiana na wapinzani wa serikali ya Syria kuua raia wa mji wa Afrin

Hata hivyo Uturuki bado imeendelea na operesheni hizo ambazo hadi sasa zimesababisha mauaji makubwa ya raia wa kawaida na askari wa Utuki na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu katika eneo hilo. 

Tags