Katibu Mkuu wa UN atahadahrisha kuhusu hali mbaya nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i42600-katibu_mkuu_wa_un_atahadahrisha_kuhusu_hali_mbaya_nchini_yemen
Huku Saudia Arabia ikiendeleza hujuma zake za kinyama dhidi ya Yemen, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametahadharisha kuhusu hali mbaya ya kibinadamu katika nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 03, 2018 09:25 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN atahadahrisha kuhusu hali mbaya nchini Yemen

Huku Saudia Arabia ikiendeleza hujuma zake za kinyama dhidi ya Yemen, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametahadharisha kuhusu hali mbaya ya kibinadamu katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Akizungumza mjini Geneva hii leo katika mkutano wa kimataifa wa kutafuta msaada wa dola bilioni tatu kwa ajili ya kusaidia Yemen, Gutteres ametoa wito wa kuondolewa mzingiro nchini humo ili kuruhusu misaada ya kibinadamu na bidhaa za kibiashara kuingia nchini humo. Amesema sehemu za kuingizia bidhaa hasa viwanja na ndege na bandari zinapaswa kuwa wazi ili kuondoa vizingiti vya misaada kuwafikia wanaohitajia. Saudi Arabia na waitifaki wake wameweka mzingiro wa baharini, nchi kavu na angani dhidi ya Yemen tokea mwezi Novemba mwaka 2017.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ametoa wito kwa pande zote katika mgogoro wa Yemen kufanya mazungumzo na mjumbe wake mpya nchini humo, Martin Griffiths bila kuchelewa.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa Wayemen milioni 22.2 wanahitajia msaada wa dharura wa chakula huku wengine milioni 8.4 wakiwa katika tishio la kukumbwa na njaa.

Watoto ni waathirika wakuu wa hujuma ya Saudia dhidi ya Yemen

Ikumbukwe kuwa Saudia ilianzisha hujuma yake dhidi ya Yemen mnamo Machi mwaka 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kuirejesha serikali kibaraka ya Abdu Rabuh Mansour Hadi aliyejiuzulu urais na kukimbilia mji mkuu wa Saudia, Riyadh. 

Raia zaidi ya elfu 14  wa Yemen wameuawa, hasa wanawake na watoto, na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika uvamizi huo wa kijeshi. Aidha watu karibu milioni moja wameambukizwa ugonjwa wa kipindupindu kote nchini Yemen huku wengine karibu 3,000 wakifariki dunia tokea mwezi Aprili mwaka jana. Mamilioni ya Wayemen pia wamepoteza makazi yao kutokana na hujuma hizo za Saudia. 

Wizara ya Haki za Binadamu Yemen ilitangaza Machi 25 kuwa kwa ujumla hujuma ya Saudia dhidi ya nchi hiyo imepelekea watu 600,000 kuuawa shahidi na kujeruhiwa.

Saudi Arabia imeshindwa kufikia malengo yake Yemen pamoja na kuwa imetumia mabilioni ya dola sambamba na kupata msaada mkubwa wa waitifaki wake katika eneo na madola ya Magharibi.