HRW: Wakuu wa Israel waliamuru mauaji ya Wapalestina Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i42614-hrw_wakuu_wa_israel_waliamuru_mauaji_ya_wapalestina_gaza
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limelaani vikali hatua ya utawala haramu wa Israel kuwaua Wapalestina waliokuwa wakiandamana kwa amani siku ya Ijumaa katika Ukanda wa Ghaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 03, 2018 22:00 UTC
  • HRW: Wakuu wa Israel waliamuru mauaji ya Wapalestina Gaza

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limelaani vikali hatua ya utawala haramu wa Israel kuwaua Wapalestina waliokuwa wakiandamana kwa amani siku ya Ijumaa katika Ukanda wa Ghaza.

Katika taarifa, HRW imesema mauaji hayo ni kinyume cha sheria na yalitekelezwa kwa makusudi kufuatia amri ya viongozi wa utawala haramu wa Israel ambao waliwataka wanajeshi kuwafyatulia risasi waandamanaji.

HRW imesema kabla na baada ya muaji ya Wapalestina 17 waliokuwa wakiandamana kwa amani katika Siku ya Ardhi, wakuu wa Israel walitamka hadharani kuwa wanajeshi wamepewa amri ya kuwafyatulia risasi Wapalestina watakaofika katika eneo la mpaka wa Ghaza na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel. Ripoti hiyo imesema idadi kubwa ya waliojeruhiwa, takribani 1,400, ni ishara kuwa utawala huo wa Kizayuni uliwapa ruhusa wanajeshi kuwapiga risasi Wapalestina ambao hawakua ni tishio lolote. Ripoti hiyo imesema mbinu hizo ni kinyume cha sheria za kimataifa na ni ishara ya tabia ya muda mrefu ya kutojali sheria iliyoko katika majeshi ya utawala wa Israel.

Sheikh Saleh al-Fawzan wa Saudi Arabia ambaye Jeshi la Israel limesema limetegemea fatuwa yake ya kupiga marufuku maandamano 

Mbali na hayo, Jeshi la Utawala wa Kizayuni wa Israel linasema linawaua Wapalestina wanaoandamana kwa kutegemea fatuwa ya mashekhe wa Kiwahhabi kutoka Saudi Arabia.

Akizungumza Ijumaa, msemaji wa jeshi la utawala haramu wa Israel Avichay Adraee aliashiria fatuwa ya shekhe maarufu wa Saudia Saleh al-Fawzan ambaye alisema maandamano ya hadhara hupelekea Waislamu wawe makafiri. Mwanazuoni huyo wa Saudia, ametoa fatuwa ya kupiga marufuku maandamano na migomo, na kudai kwamba tabia kama hiyo inakiuka maadili ya Waislamu na kuwa ni sifa ya makafiri.