Jihad Islami: Mrithi wa Ufalme wa Saudia amesaliti malengo ya Palestina
Msemaji wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina amesema hatua ya Mrithi wa Ufalme wa Saudia Mohammad bin Salman kuutambua utawala bandia wa Israel ni usaliti mkubwa kwa malengo matukufu ya Palestina.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Bin Salman ameongeza kasi ya mkakati wa Saudia kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel huku akipuuza haki na malengo matukufu ya harakati ya kupigania ukombozi wa Palestina ikiwa ni pamoja na kukombolewa mji wa Quds ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu. Katika mahojiano na Jarida la Atlantic la Marekani, Bin Salman amesema Saudia na utawala haramu wa Israel zina maslahi ya pamoja na iwapo zitakuwa na uhusiano wa wazi, basi utawala huo bandia utapata faida kubwa na pia nchi za Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi nazo zitafaidika.
Akijibu matamshi hayo, Msemaji wa Jihad Islami Daoud Shahab amelaani vikali matamshi ya Bin Salman ya kuutambua utawala bandia wa Israel na kusema: "Hakuna shaka kuwa lengo la Saudia la kuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel ni kujaribu kujipendekeza kwa Marekani."
Msemaji wa Jihad Islami amesema kuna udharura wa Waarabu na Waislamu kwa jumla kufahamishwa ukweli na uhalisi wa mambo kuhusu mapambano ya Wapalestina ya kutetea haki yao. Amesema maandamano ya Ijumaa ya Wapalestina ya kutaka kurejea katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na Israel ni sawa na mwamko ulioshuhudiwa katika nchi za Kiarabu miaka ya hivi karibuni.
Katika maandamano hayo wanajeshi katili wa Israel waliwaua Wapalestina wapatao 18 na kuwajeruhi mamia ya wengine lakini katika mahojaino yake na Jarida la Atlantic la Marekani, mrithi wa ufalme wa Saudia hakugusia hata kidogo ukatili huo ambao umelaaniwa kote duniani.
Mwezi uliopita, katika mkakati wake wa kuboresha uhusiano na utawala bandia wa Israel, Saudi Arabia iliruhusu ndege zinazoenda au kutoka Israel kupita katika anga yake.
Katika miezi ya hivi karibuni nchi za kadhaa za Kiarabu zikiongozwa na Saudia zimekuwa mbioni kuanzisha uhusiano wa karibu na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ni adui nambari moja wa nchi za Kiislamu duniani.