Harakati za kigaidi za Imarati nchini Yemen
(last modified Sun, 08 Apr 2018 06:59:11 GMT )
Apr 08, 2018 06:59 UTC
  • Harakati za kigaidi za Imarati nchini Yemen

Afisa mmoja wa ngazi za juu wa usalama katika mkoa wa Aden, kusini mwa Yemen amefichua kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati inafanya mauaji makubwa katika mkoa huo kama njia ya kuzidi kujipenyeza Abu Dhabi huko kusini mwa Yemen na jitihada zake za kutaka kuigawa nchi hiyo ya Kiarabu.

Shirika la habari la Associated Press la nchini Marekani limemnukuu afisa usalama wa ngazi za juu huko Aden akifichua kuwa Imarati imejipenyeza Yemen kwa kutumia makundi ya kigaidi ya al Qaida na Daesh ili kupigana vita na Harakati ya Wananchi ya Yemen ya Ansarullah; na hadi sasa Imarati imeshauwa maimamu wa sala za jamaa wasiopungua 20 katika mji wa Aden kupitia makundi hayo ya ukufurishaji yenye misimamo ya kufurutu ada. Miji ya kusini mwa Yemen imekuwa katika hali ya machafuko na ukosefu wa amani tangu mwezi Machi mwaka 2015 wakati Saudia na baadhi ya nchi nyingine waitifaki wake ikiwemo Imarati zilipoishambulia Yemen kwa kisingizio cha kutaka kumrejesha madarakani kibaraka wao Abdu Rabbu Mansour Hadi Rais wa Yemen aliyejiuzulu.

Rais mstaafu wa Yemen, Abdu Rabbu Mansour Hadi 

Kuwepo makundi ya kigaidi yakiwemo al Qaida na Daesh huko kusini mwa Yemen kumevuruga usalama katika maeneo hayo. Hivi sasa Imarati inavamia na kuyadhibiti maeneo tajiri kwa mafuta pia huko Yemen kwa kuwatumia wanajeshi 3000 iliyowaajiri; ambapo imeelezwa kuwa maeneo hayo yana visima vya mafuta na yamevamiwa lengo likiwa ni kuyatenganisha maeneo hayo na Yemen. Hii ni katika hali ambayo ripoti mbalimbali zimeweka wazi kuhusika pakubwa Imarati katika kuasisi na kuenea makundi ya kigaidi huko kusini mwa Yemen; jambo linaloashiria fitina ya waziwazi inayofanywa na Imarati katika eneo la Mashariki ya Kati ikiwemo huko Yemen. 

Baada ya Saudi Arabia tunaweza kusema kuwa Imarati imehusika pakubwa katika kuibua fitina na njama katika eneo hilo ikiwemo huko Yemen. Katika fremu hiyo, Imarati ilifikia mapatano na Rais mstaafu wa Yemen Abdu Rabbu Mansour Hadi, ambapo rais huyo aliikodisha Imarati visiwa viwili vya Yemen kwa muda wa miaka 99. Aidha kupitia hila na njama hizo, Imarati inaendeleza mkondo huo wa siasa za madola yanayopenda kujitanua ya Magharibi hususan Marekani ili kuigawa Yemen.

Watawala wa nchi za Kiarabu wanafuatilia malengo mbalimbali katika kalibu ya matukio yanayojiri kwenye eneo hili kwa kustafidi na ugaidi na kuwatumia mamluki wao ili kufanikisha malengo yao haramu.

Televisheni ya al Mayadeen imeripoti kuwa nyaraka mbalimbali zinaonyesha kwamba Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia na Muhammad bin Zaid Aal Nahyan mrithi wa mtawala wa Abu Dhabi wanawasaidia baadhi ya viongozi wa makundi ya kigaidi ya al Qaida na Daesh huko Yemen. 

Muhammad bin Zaid al Nahyan na akiwa na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman 

Katika nyaraka hizo zilizofichuliwa, Adam Zubin mmoja wa maafisa wa wakati huo wa Wizara ya Fedha ya Marekani  anayehusika na masuala ya ugaidi amenukuliwa akisema kuwa: Bin Salman na bin Zaid walikuwa na uhusiano wa muda mrefu na Ali Abker al Hassan na Abdullah Faisal al Ahdal raia wa Yemen ambao majina yao yapo kwenye orodha ya Marekani ya watu wenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida. 

Matukio ya Yemen yanaonyesha kuwa, mgogoro wa nchi hiyo uko katika mkondo wa hatari zaidi na wakati huo huo tata zaidi kufuatia uingiliaji wa serikali kama Saudi Arabia na Imarati.