Takriban watoto 239 wamefariki dunia magharibi mwa Sudan tangu Januari
(last modified Mon, 30 Jun 2025 08:00:21 GMT )
Jun 30, 2025 08:00 UTC
  • Takriban watoto 239 wamefariki dunia magharibi mwa Sudan tangu Januari

Takriban watoto 239 wameaga dunia magharibi mwa Sudan tangu mwezi Januari mwaka huu kutokana na ukosefu wa chakula na dawa za kutosha. Ripoti hii imetolewa na Mtandao wa Madaktari wa Sudan.

Taasisi hiyo ya tiba ya kiraia imesema katika taarifa yake kuwa timu yake imesajili idadi ya watoto walioaga dunia kutokana na utapiamlo na uhaba mkubwa wa chakula na vifaa vya matibabu katika mji wa El Fasher, makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini kati ya Januari na Juni.

Aidha imetahadharisha kuhusu kuongezeka ukosefu wa chakula na kuendelea kuwshambuliwa nyumba zinazowahudumia watoto wanaopatiwa matibabu ya lishe katika mji wa El Fasher ambao unaendelea kuzingirwa na wanamgambo wa kikosi cha msaada wa haraka (RSF).

Mtandao wa Madaktari wa Sudan umesema unasikitishwa na kitendo cha jamii ya kimataifa cha kuwapuuza watoto wa Darfur ambao wamevumilia mateso huku wakiwa chini ya mzingiro wa zaidi ya mwaka mmoja sasa.  

Umesema hatua za haraka zinahitajika ili kufunua korido za kibinadamu, kuruhusu usambazaji wa misaada ya dharura ya kibinadamu na ya kitiba na kuondoa mzingiro katika mji wa El Fasher. 

Mapigano kati ya jeshi la Sudan na wamnamgambo wa RSF yameutikisa mji wa El Fasher tangu Mei 10 mwaka huu, licha ya indhari ya kimataifa kuhusu vita katika mji huo, ambao unatumika kama kitovu kikuu cha operesheni za kibinadamu katika majimbo matano ya jimbo la Darfur huko Sudan.