Dec 02, 2023 04:20 UTC
  • Jumamosi, 02 Disemba, 2023

Leo ni Jumamosi 18 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1445 Hijria mwafaka na tarehe Pili Disemba, 2023 Miladia

Katika siku kama ya leo miaka 1117 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Ahmad bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Abdu Rabbuh mshairi na mwandishi mahiri wa Kiarabu. Abdu Rabbuh alibobea mno katika mashairi. Kitabu mashuhuri zaidi cha msomi huyo ni al Iqdul Fariid ambacho kinahusiana na historia, lugha na mashairi. ***

Ahmad bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Abdu Rabbuh

 

Katika siku kama ya leo miaka 995 iliyopita, Abu al-Abbas Ahmad bin Ali maarufu kwa jina la Najjashi aliaga dunia huko Samarra, Iraq akiwa na umri wa miaka 78. Najjashi alikuwa alimu na msomi mkubwa katika karne ya tano Hijria na alibobea na kutabahari katika elimu ya hadithi na wapokezi wa hadithi. Kitabu cha Rijali ni miongoni mwa vitabu muhimu vya msomi huyo wa Kiislamu. ***

Abu al-Abbas Ahmad bin Ali maarufu kwa jina la Najjashi

 

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, Mirza Kuchak Khan Jangali, mwanaharakati na mpigania ukombozi wa Kiirani aliuawa shahidi na vibaraka wa Reza Khan, dikteta wa wakati huo wa Iran kwa ushirikiano wa madola ya Umoja wa Kisovieti na Uingereza. Mirza Kuchak Khan Jangali alijifunza masomo ya dini akiwa katika rika la ujana na kufanikiwa kukwea daraja za juu za kielimu. Baadaye alijiunga na safu ya wapigania uhuru hadi alipokamatwa na vibaraka wa Reza Khan na kuuawa kwa kukatwa kichwa kilichopelekwa kwa mfalme huyo kibaraka. ***

Mirza Kuchak Khan Jangali

 

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, Peninsula ya Korea iligawanywa katika sehemu mbili za kaskazini na kusini. Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia na kushindwa Japan ambayo ilikuwa imedhibiti sehemu kubwa ya maeneo ya mashariki mwa Asia, viongozi waitifaki walifanya vikao katika miji ya Yalta na Potsdam wakijadili juu ya namna ya kuongoza dunia baada ya kumalizika kwa vita hivyo. Hata hivyo katika vikao hivyo kulibainika mapema kwamba Marekani na Urusi ya Mazani, zilikuwa zikiwania fungu kubwa zaidi kwa ajili ya kupenyeza siasa zao na kulidhibiti eneo tajwa. Hivyo eneo hilo na kwa mujibu wa mapendekezo ya viongozi wa nchi zilizoibuka washindi katika vita, likagawanywa sehemu mbili katika siku kama ya leo. ***

Korea Kaskazini na Kusini

 

Miaka 69 iliyopita katika siku kama ya leo, Laos ilipata uhuru kamili. Uhuru wa nchi hiyo ulipasishwa katika mkutano uliofanyika Geneva mwaka 1945 kwa kuhudhuriwa na nchi za eneo na serikali kubwa duniani. Laos ilikuwa chini ya uongozi rasmi wa Ufaransa tangu mwaka 1893. Na ilipofika mwaka 1949, Ufaransa ililazimika kuipatia Laos uhuru wa kiwango fulani katika fremu ya Umoja wa Kifaransa, kufuatia mapambano ya ukombozi yaliyoanzishwa katika eneo la India na China. ***

Bendera ya Laos

 

Katika siku kama ya leo Miaka 67 iliyopita, Fidel Castro alianzisha harakati ya kuikomboa nchi yake ya Cuba. Castro akiwa na lengo la kupambana na dikteta Fulgencio Batista, alianzisha mapambano ya silaha akiwa pamoja na wenzake kwa kuishambulia kambi ya kijeshi ya Moncada. Hata hivyo vikosi vya dikteta Batista viliikandamiza vibaya harakati hiyo na kumtia mbaroni Fidel Castro na kumfunga jela. Baada ya muda Castro alipelekwa uhamishoni. Hata hivyo baadaye aliunda kundi jingine la wapiganaji na kurejea Cuba alikoanzisha mapambano mapya. Hatimaye wanamapinduzi hao wa Cuba walifanikiwa kuyadhibiti maeneo muhimu ya nchi hiyo hali iliyomfanya dikteta Fulgencio Batista akimbilie katika kituo cha kijeshi cha Marekani na baadaye kutoroka nchi hiyo. ***

Fidel Castro

 

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, Umoja wa Falme za Kiarabu ulipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza na kila inapowadia siku kama hii ya leo nchi hiyo huiadhimisha kama siku ya taifa. Ni vyema kutaja hapa kuwa, tawala za kifalme za kusini mwa Ghuba ya Uajemi zilikuwa chini ya utawala wa Uingereza tangu mwaka 1920 Miladia. Uingereza iliasisi vituo vingi vya kijeshi katika eneo hilo, hata hivyo baada ya Vita vya Pili vya Dunia, nchi hiyo ilidhoofika na ikaliweka katika ajenda yake suala la kuondoka katika Ghuba ya Uajemi. ***

Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati)

 

Na tarehe Pili Disemba kila mwaka huadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Kufutwa Utumwa kote duniani. Japokuwa utumwa umefutwa katika maeneo mengi ya dunia lakini suala hilo lingali linashuhudiwa duniani katika kalibu ya utumwa mambo leo. ***

Siku ya Kimataifa ya kufutwa utumwa

 

Tags