Saudi Arabia yaendelea kuishambulia Yemen kwa mabomu yaliyopigwa marufuku
Saudi Arabia imeendelea na hujuma zake za kijeshi huko Yemen na kuendelea kutumia mabomu yaliyopigwa marufuku kimataifa.
Kanali ya Televisheni ya al-Masirah imetangaza kuwa, ndege za kijeshi za Saudi Arabia leo zimeyashambulia kwa mabomu yaliyopigwa marufuku ya vishada maeneo ya uwanja wa ndege wa Sa'dah na kituo cha kijeshi cha Kahlan kaskazini mwa Yemen.
Saudi imefanya mashambulio hayo ikitumia mabomu hayo hatari ambayo yamepigwa marufuku kimataifa. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekuwa likiitaka Saudi Arabia iache kutumia mabomu ya vishada dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen.
Hivi karibuni shirika la Human Rights Watch lililaani vikali hatua ya Saudi Arabia ya kendelea kutumia mabomu ya vishada na kueleza kwamba, kwa mujibu wa mkataba wa silaha wa mwaka 2008 matumizi ya mabomu hayo yamepigwa marufuku.
Hadi sasa nchi 108 duniani zimetia saini mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya mabomu hatari ya vishada.
Saudi Arabia ilianzisha hujuma yake ya kijeshi dhidi ya Yemen mnamo Machi mwaka 2015 kwa lengo la kuirejesha madarakani serikali kibaraka ya Abdu Rabuh Mansour Hadi aliyejiuzulu urais na kukimbilia katika mji mkuu wa Saudia, Riyadh.
Raia zaidi ya elfu 14 wa Yemen wameuawa, hasa wanawake na watoto, na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika uvamizi huo wa kijeshi. Aidha mamilioni ya Wayemen pia wamepoteza makazi yao kutokana na hujuma hizo za Saudi Arabia na washirika wake.