Iran: UN ikome kuupendelea utawala haramu wa Israel
Mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa utawala ghasibu wa Israel ndio unaovuruga amani na usalama wa Mashariki ya Kati na amelitaka Baraza la Usalama la umoja huo kukoma kuupendelea utawala wa Kizayuni wa Israel.
Gholam-Ali Khoshroo amekiambia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichokutana jana jioni kujadili hali ya Mashariki ya Kati na kadhia ya Palestina hususan mauaji yaliyofanywa na Israel dhidi ya waandamanaji katika eneo la Ukanda wa Gaza kwamba: Iwapo Baraza la Usalama lina azma ya kweli ya kutaka kurejesha amani na usalama eneo la Mashariki ya Kati halina budi kutupilia mbali sera zake za kuipendelea Israel. Khoshroo amesema hatua ya Israel ya kuivamia na kuikalia kwa mabavu Palestina ndiyo sababu kuu ya ghasia na mivutano ya Mashariki ya Kati.
Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameashiria pia hatua ya Israel ya kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi ya Syria huko Golan na kusema kuwa, hatua hiyo inakiuka sheria za kimataifa na kwamba imechukuliwa kwa ajili ya kuyaunga mkono na kuyasaidia makundi ya kigaidi.
Vilevile amesema kuwa uamuzi wa Marekani wa kuhamishia ubalozi wake katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds huko Palestina unakiuka sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza Kuu na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwamba hatua hiyo imechochea zaidi mgogoro wa Mashariki ya Kati.