Sisitizo la Erdoğan la kuwekewa vikwazo vya kiuchumi Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i44988-sisitizo_la_erdoğan_la_kuwekewa_vikwazo_vya_kiuchumi_israel
Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa, kwa mujibu wa maamuzi yaliyochukuliwa katika kikao cha dharura cha nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC mjini Istanbul, kulitakiwa kuanza kutekelezwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya utawala katili wa Kizayuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 26, 2018 03:09 UTC
  • Sisitizo la Erdoğan la kuwekewa vikwazo vya kiuchumi Israel

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa, kwa mujibu wa maamuzi yaliyochukuliwa katika kikao cha dharura cha nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC mjini Istanbul, kulitakiwa kuanza kutekelezwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya utawala katili wa Kizayuni.

Rais Erdoğan sambamba na kuashiria kikao cha wiki jana cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC mjini Istanbul Uturuki, kufuatia hatua ya Marekani ya kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv na kuupeleka mjini Quds, (Jerusalem), amesema kuwa jumuiya hiyo imeazimia kuziwekea mashinikizo na vikwazo nchi ambazo zitafuata maamuzi ya Marekani katika uwanja huo. Aidha rais huyo wa Uturuki amesisitiza kuwa, maamuzi ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuuhamishia ubalozi wa nchi yake mjini Quds haitaweza kubadilisha uhalisia huu kwamba mji huo ni mji mkuu wa taifa la Palestina na si vinginevyo.

Mauaji ya kutisha yanayofanywa na utawala katili wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina

Ameongeza kuwa, hatua hiyo ya Trump imeipotezea tu itibari Washington kwa sababu kwa mujibu wa upigajikura uliofanywa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala hilo, ilibainika wazi kuwa dunia nzima haikubaliani hata kidogo na maamuzi ya Trump kuhusiana na suala hilo. Matamshi ya Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki yanaonyesha uwepo wa mtazamo mpya kati ya nchi za Kiislamu ambao iwapo utatekelezwa vilivyo na nchi hizo, basi unaweza kuuwekea mashinikizo utawala huo khabithi wa Israel.

Wakati jinai dhidi ya Wapalestina zikijiri, Erdogan tayari alikuwa na mahusiano mazuri na Israel

Hii ikiwa na maana kwamba, lau kama nchi za Kiislamu zingeamua kushirikiana chini ya bendera moja na kuuwekea vikwazo vya kisiasa na kiuchumi utawala huo, zingepelekea kuongezeka wimbi la kutengwa utawala huo katika ngazi za kieneo na kimataifa. Kadhalika nchi za Kiislamu zinaweza kutumia nafasi yao kuyashawishi mataifa mengine huru ya dunia kushirikiana nazo katika uwanja huo. Hususan wakati huu ambapo kunashuhudiwa wimbi la uungaji mkono wa wananchi kwa taifa madhlumu la Palestina hata katika mataifa ya Ulaya. Hivyo kuna udharura wa mataifa ya Kiislamu kuimarisha umoja wao katika kuelekeza mashinikizo zaidi dhidi ya utawala huo wa kimabavu.

Netanyahu na Shimon Peres, wakipongeza ushirikiano mzuri kati yao na Uturuki

Hata hivyo ukweli ambao hauwezi kufumbiwa macho ni kwamba, katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, mataifa ya Kiislamu ukitoa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, yalipanua wigo wa mahusiano yao ya kibiashara na kiuchumi na utawala huo wa Israel ambapo Uturuki ni moja ya nchi za Kiislamu ambazo zimekuwa zikisisitiza kuimarisha mahusiano hayo ya kiuchumi na kidiplomasia na Tel Aviv. Nyaraka mbalimbali zinaonyesha kwamba katika miaka kadhaa iliyopita, Uturuki ndio nchi pekee ambayo iliishia tu kutoa matamko na pengine makali na ya kisiasa kuuhusu utawala haramu wa Kizayuni ambapo haikuwa tayari kuchukua hatua zozote za kivitendo katika uwanja huo. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, mahusiano ya kiuchumi kati ya utawala wa Kizayuni na Ankara yameendelea kuongezeka na kupindukia kiwango cha Dola bilioni nne.

Kulia ni Berat Albaytak, Waziri wa Nishati wa Uturuki na Waziri wa Nishati wa Israel Yuval Steinitz

Kuhusiana na suala hilo, mwandishi lhan Güllü amenukuliwa akisema kwamba: "Kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita hakuna suala lolote la kisiasa lililoweza kuathiri mahusiano ya kibiashara na kiuchumi kati ya Uturuki na utawala bandia wa Israel. Hata kipindi ambacho Uturuki ilionyesha mtazamo wa kisiasa kwamba ina mgogoro na Israel, lakini bado kwa mtazamo wa kiuchumi iliendelea kupanua mahusiano yake na utawala huo." Mwisho wa kunukuu. Kwa mitazamo hiyo ya undumakuwili, itakuwa ni vigumu sana kwa nchi za Kiislamu kuweza kufikia malengo yao kuhusu utawala haramu wa Kizayuni. Suala muhimu ni hili kwamba iwapo kweli Uturuki imeazimia kuuwekea mashinikizo utawala huo wa kibaguzi, kwanza kabisa inatakiwa kupunguza mahusiano yake ya kibiashara na Israel na kinyume na hali hiyo Ankara haitoweza kuwakinaisha Waislamu duniani kwamba kweli ni mtetezi wa haki za Wapalestina.