Jul 07, 2018 02:42 UTC
  • Tsunami ya kamatakamata nchini Saudi Arabia

Vita vya madaraka katika ukoo wa Aal Sad nchini Saudi Arabia vinachukua mkondo mpya na mpana zaidi kila siku ambapo wanawafalme na maafisa wengi wa ngazi za juu nchini humo wamekuwa wakitiwa mbaroni kwa amri ya Muhamm bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa nchi hiyo.

Kuhusu suala hilo gazeti la Wall Street Journal la nchini Marekani limeandika katika toleo lake la hivi karibuni kwamba viongozi wa Saudia wamekamata makumi ya wanawafalme na wafanyabiashara mashuhuri na kuwafungia katika jela moja ya siri iliyoko karibu na Riyadh, mji mkuu wa nchi hiyo. Tokea baba yake Salman bin Abdul Aziz, achukue kiti cha ufalme wa Saudia mnamo Junuari 2015, Muhammad bin Salman ambaye hakuwa akijulikana vizuri nchini humo ametokea kuwa mtu aliye na madaraka makubwa na anayechukua maamuzi yote muhimu ya kiserikali nchini. Uchu wa madaraka wa Bin Salman umekuwa ukiandamana na uvunjaji wa desturi na mila za nchi hiyo, mfano wa wazi ukiwa ni hatua yake ya kutwaa nafasi ya mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, kutoka kwa mrithi mstahiki wa nafasi hiyo na ambaye alikuwa angali hai yaani, Muhammad bin Naif.

Muhammad bin Naif (kulia) aliyepokonywa madaraka na Muhammad bin Salman (kushoto)

Muhammad bin Salman anafanya kila analoweza ili kuwafuta washindani na wapinzani wake wote wanaoweza kumzuia kuchukua ufalme wa Saudia. Mmoja wa wapinzani hao mashuhuri ni mwanamfalme Turki bin Abdullah mwana wa Abdullah bin Aziz, mfalme wa zamani wa nchi hiyo, ambaye alitiwa mbaroni katika wimbi la kwanza la kamatakamata hiyo. Mpinzani mwingine ni mwanaflme Abdul Aziz mwana wa kiume wa Fahd bin Abdul Aziz, mfalme mwingine wa zamani wa nchi hiyo inayoendeshwa kwa misingi ya kiukoo na kifamilia. Kwa mujibu wa tovuti ya Hail Times, utawala wa Saudia Arabia ni utawala wa kidikteta unaolegalega na usiokuwa na uwazi, ambao haujiamini hata kidogo katika uendeshaji wa mambo ya nchi. Hii ndio maana umehodhi madaraka yote na kuyaweka mikononi mwa familia ya Aal Salman pamoja na kutekeleza ukandamizaji mkubwa wa kisiasa nchini. Kuhusiana na suala hilo Samaah al-At'fi, mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kisasa mjini London pia anasema kwamba tokea Muhammad bin Salman achukue nafasi ya mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, amewatia mbaroni wapinzani 4000 na wakati huohuo kupiga marufuku shughuli za mitandao 14 ya upinzani nchini humo.

Baadhi ya wanawafalme wa Saudia waliotiwa mbaroni na Muhammad bin Salman

Mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudia anaamini kwamba njia pekee ya kumuwezesha kufikia ufalme wa nchi hiyo ni kuwakandamiza wapinzani, kuwaweka korokoroni na kufanya marekebisho ya kimaonyesho katika nyanja za kiuchumi na kijamii. Ni katika mazingira hayo ndipo tukashuhudia ufyatuaji risasi katika kasri ya ufalme mjini Riyadh na kumpelekea Muhammad bin Salman kutoweka kwa wiki kadhaa na kwa namna ya kutiliwa shaka katika uwanja wa kisiasa wa Saudia. Kwa kuandaa mazingira hayo ya kuzua hofu na ya kipolisi nchini, mrithi huyo wa kiti cha ufalme amekuwa akitafuta fursa ya kufanya mabadiliko makubwa ya kisiasa ili kujiaandalia mazingira ya kuweza kuketi kwenye kiti cha ufalme wa nchi hiyo. Matukio ya baada ya mwanamfalme huyo kutoweka kwa wiki kadhaa katika uwanja wa kisiasa wa Saudia kufuatia tukio la ufyatuaji risasi katika kasri ya mjini Riyadh, na ambayo yamefuatiwa na kamatakamata inayoendelea hivi sasa katika nchi hiyo ya kifalme, ni mambo yanayotilia nguvu dhana hii kwamba Muhammad bin Salman anatumia kila mbinu ili kuweza kuchukua madaraka ya nchi hiyo.

Tags