EurAsian Times: NATO ya Kiarabu dhidi ya Iran, itaishia kushindwa
Gazeti la EurAsian Times limeandika kuwa, fedha za Saudia, silaha za Marekani na vyombo vya upelelezi vya Israel, vinaunda muungano dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kifupi 'NATO ya Kiarabu.'
Nato hiyo ya Kiarabu ambayo imeratibiwa na Marekani, inazijumuisha Saudi Arabia, Imarati, Bahrain, Kuwait, Qatar, Misri na Jordan. Mwezi Oktoba mwaka huu, Marekani imepanga kuitisha kikao kitakachojadili suala la Nato hiyo ya Kiarabu ambapo inataka kwa kutumia njia hiyo, iweze kudhibiti zaidi eneo la Mashariki ya Kati. Weledi wa mambo wanaamini kwamba nchi nyingi za Kiarabu hazina siasa za usalama za pande mbili kama ambavyo pia hazina adui wa pamoja katika eneo hilo, na kwamba Marekani inajitahidi kuzishawishi nchi hizo kuiona Iran kuwa adui yao. Darko Lazar, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa nchini Lebanon anasema kuwa, mipango yenye kushabihiana ya serikali ya Marekani kwa ajili ya kufanikisha na kuanzisha muungano wa kijeshi kwa kuwashirikisha waitifaki wake wa Kiarabu dhidi ya Iran, itaishia kufeli.
Kwa mujibu wa Lazar, NATO ya Kiarabu, ni mpango wa Kimarekani na Saudia ambao umeratibiwa kwa umakini, ambapo Riyadh itatakiwa kudhamini fedha, Washington kudhamini silaha, Misri kudhamini askari na Israel kudhamini taarifa za upelelezi. Hata hivyo kuwepo baadhi ya tofauti kati ya tawala za Kiarabu, kumewafanya weledi wengi wa mambo kufikia natija hii kwamba, ni suala lililo mbali kuweza kuunda muungano wa majeshi ya Kiarabu chini ya bendera moja. Hii ni kusema kuwa, hadi sasa Wasaudi hawawezi kujitegemea. Katika uwanja huo hata ndege zake za kijeshi zinarushwa na marubani wa Pakistan na Misri katika hali ambayo askari wengine vibaraka kutoka nchi za kigeni wamekwisha poteza maisha yao katika kutetea mipaka ya kusini mwa Saudia.