Hizbullah: Saudia inakwamisha kuundwa serikali mpya nchini Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47256-hizbullah_saudia_inakwamisha_kuundwa_serikali_mpya_nchini_lebanon
Naibu wa Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, kitendo cha baadhi ya mirengo ya kisiasa inayochochewa na Saudi Arabia, cha kushikilia misimamo yao ya kupewa nafasi maalumu serikalini ndicho kinachokwamisha kuundwa serikali mpya nchini Lebanon.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 05, 2018 20:50 UTC
  • Hizbullah: Saudia inakwamisha kuundwa serikali mpya nchini Lebanon

Naibu wa Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, kitendo cha baadhi ya mirengo ya kisiasa inayochochewa na Saudi Arabia, cha kushikilia misimamo yao ya kupewa nafasi maalumu serikalini ndicho kinachokwamisha kuundwa serikali mpya nchini Lebanon.

Sheikh Ali Damoush amesema kuwa, kile kinachoshuhudiwa hivi sasa ni hatua za makusudi za Saudi Arabia za kukwamisha kuundwa serikali nchini Lebanon kwa mgongo wa baadhi ya mirengo ya kisiasa inayoshikilia misimamo isiyoingia akilini ya kutaka kupewa nafasi maalumu serikalini kinyume na hali halisi ilivyo.

Hata hivyo amesema, wananchi waaminifu wa Lebanon wanahitajia kuwa na serikali ambayo itaweza kuwatatulia matatizo mengi waliyo nayo na kuongeza uimara na kusimama kwake kidete hasa kwa kuzingatia kuwa baadhi ya wananchi wa Lebanon hawana imani tena na wanasiasa.

Wanajeshi wa Israel walipata kipigo kikali kutoka kwa Hizbullah walipoanzisha vita dhidi ya Lebanon mwaka 2006

 

Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa, katika vita vya siku 33 vya mwaka 2006, utawala wa Kizayuni ulitumia nguvu zake zote za kijeshi na kisiasa kwa shabaha ya kuudhofisha muqawama lakini muqawama ulithibitisha vizuri nguvu zake kwa kutoa kipigo cha kuifedhehesha Israel na waitifaki wake kwenye vita hivyo.

Vile vile amesema, utawala wa Kizayuni unaogopa sana kuanzisha vita vingine na Lebanon kutokana na kwamba unatambua vyema kuwa, muqawama una nguvu na hivi sasa umezidi kuwa na nguvu kutokana na vita vya Syria.