Bomu lililotumika kuua watoto Yemen liliundwa Marekani
Wataalamu wa silaha wamethibitisha kuwa bomu ambalo lilitumiwa na ndege za kivita za Saudia hivi karibuni kushambulia basi la shule na kuua makumi ya watoto lilitengenezwa Marekani.
Wataalamu wakizungumza na televisheni ya CNN wamesema bomu ambalo lilitumika katika hujuma hiyo lina uzito wa pauni 500 au kilo 227 na ni aina ya MK 82 lililoundwa na shirika la zana za kivita la Marekani la Lockheed Martin.
Itakumbukwa kuwa Alkhamisi 9 Agosti ndege za kivita za utawala dhalimu wa Saudia zilishambulia basi lililokuwa na watoto wadogo katika mji wa Dhahyan, mkoani Sa'ada, kaskazini mwa Yemen na kuua kikatili watu 51 wakiwemo watoto 40 na kujeruhi wengine karibu ya 80. Vyombo vya habari nchini Yemen vimesema kuwa watoto hao walikuwa vijana wa shule waliokuwa wakirejea nyumbani baada ya kuhudhuria masomo ya Qur'ani Tukufu ya majira ya joto.
Shambulizi hilo linaendelea kulaaniwa vikali na jamii ya kimataifa huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakitaka uchunguzi huru ufanyike.
Ripoti zinasema bomu hilo la MK 82 ambalo lilitumika katika jinai hiyo mkoani Sa'ada ni sawa na bomu ambalo lilitumika Oktoba 2016 katika hujuma ya Saudia dhidi ya mjumuiko wa mazishi katika ukumbi mmoja katika mji mkuu wa Yemen, Sana'a ambapo watu 155 waliuawa na wengine 525 kujeruhiwa.
Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi. Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasiopungua 15,000 wasio na hatia.