UN yakemea vikali jinai za Saudi Arabia nchini Yemen
Mwenyekiti wa Kamati ya Haki za Watoto ya Umoja wa Mataifa amesema kuwa mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na Saudi Arabia na waitifaki wake yameua watoto wengi nchini Yemen.
Raynath Winter amesema kuwa, kuna udharura wa kufanyika uchunguzi mpana na usiopendelea upande wowote kuhusu mashambulizi yanayofanywa na Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen.
Wito huo wa Mwenyekiti wa Kamati ya Haki za Watoto ya Umoja wa Mataifa umetolewa siku chache baada ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Matiafa (UNICEF) kulaani vikali hujuma ya hivi karibuni ya ndege za kivita za Saudia katika mkoa wa Hudaydha ambayo imeua watoto 26. UNICEF imeutaka utawala wa Aal Saud usitishe jinai dhidi ya watoto wa Yemen.
Jinai hiyo imefanyika takribani wiki mbili tu baada ya ndege za kivita za utawala wa Saudia kufanya shambulizi jingine la kinyama dhidi ya basi lililokuwa limebeba wanafunzi wa Qur'ani Tukufu katika eneo la Dhahiyan mkoani Saada. Watoto 55 waliuawa na wengine 77 kujeruhiwa katika shambulizi hilo.
Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi. Mashambulizi hayo yamesababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasiopungua 15,000 wasio na hatia.