Saudia yawapiga marufuku Wapalestina laki 6 kwenda kuhiji
Utawala wa Aal-Saud umewapiga marufuku Wapalestina laki sita kwenda katika mji mtakatifu wa Makka nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kushiriki ibada za Hija na Umra.
Taasisi za kushughulikia masuala ya safari za Hija na Umra nchini Jordan na Quds Mashariki inayokaliwa kwa mabavu zilitaarifiwa kuhusu marufuku hiyo mapema mwezi huu bila kupewa maelezo ya kina.
Abu Khaled al-Jimzawi, Mkurugenzi wa Ofisi ya Utalii Mashariki mwa Quds ameliambia shirika la habari la Middle East Eye kwamba, Wapalestina laki sita wanaoshi nchini Jordan bila kuwa na uraia na licha ya kuwa na pasi za kusafiria za muda walizopewa na serikali ya Jordan, lakini hawataruhusiwa kwenda kushiriki ibada ya Hija au Umra, kutokana na sheria mpya iliyotangazwa na Aal-Saud.
Vyombo vya habari vya Kiarabu vimeripoti kuwa, yumkini marufuku hiyo ya utawala wa kifalme wa Aal-Saud imetolewa kwa msingi wa kufanikisha kile Rais Donald Trump wa Marekani amekitaja kama 'Muamala wa Karne'.
Julai mwaka huu, Kamati ya Kimataifa ya Kusimamia Haram Mbili za Makka na Madina iliwasilisha barua mbili tofauti kwa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa na Kamisheni ya Kidini na Uhuru wa Kujieleza ya Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Bunge la Ulaya, ikiishitaki Saudi Arabia kwa kuingiza masuala ya siasa katika ibada ya Hija sambamba na kuweka mipaka ya uhuru wa kidini.
Hii ni baada ya watawala wa Riyadh kuwawawekea vizingiti na masharti chungu nzima raia wa Qatar na Syria waliokuwa wakitaka kwenda kutekeleza amali za Hija na Umra.