Shehe mpambe wa Bin Salman ataka kufanywa 'safari ya amani' Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i48632-shehe_mpambe_wa_bin_salman_ataka_kufanywa_'safari_ya_amani'_israel
Mwanachuoni mmoja mashuhuri ambaye ni mtu mwenye uhusiano wa karibu na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammad Bin Salman ametoa mwito wa kutumwa ujumbe wa viongozi wa 'dini tatu kuu' huko Quds tukufu inayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni, kwa lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro kati ya Palestina na Israel.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 07, 2018 04:17 UTC
  • Shehe mpambe wa Bin Salman ataka kufanywa 'safari ya amani' Israel

Mwanachuoni mmoja mashuhuri ambaye ni mtu mwenye uhusiano wa karibu na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammad Bin Salman ametoa mwito wa kutumwa ujumbe wa viongozi wa 'dini tatu kuu' huko Quds tukufu inayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni, kwa lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro kati ya Palestina na Israel.

Mohammed bin Abdul Karim Issa, Mkuu wa Jumuiya ya Ulimwengu wa Kiislamu (Muslim World League) amesema kuna haja ya kutumwa 'ujumbe wa amani' utakaowajumuisha viongozi wa dini tatu za Uislamu, Uyahudi na Ukristo kuyatembelea maeneo yote matukufu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel, kwa shabaha ya kuupatia ufumbuzi mzozo uliopo.

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa, pendekezo la msomi huyo wa Saudia mpambe wa Bin Salman ni mwendelezo wa Riyadh wa kutaka kuimarisha uhusiano wake na utawala haramu wa Israel.

Hii ni katika hali ambayo, Aprili mwaka huu, Bin Salman katika mahojiano na gazeti la Marekani la Atlantic, alisema kuwa, "Naamini kuwa kila mmoja popote pale alipo ana haki ya kuishi katika taifa lake lenye amani. Naamini kwamba Wapalestina na Waisraeli wana haki ya kuishi katika ardhi zao."

Bin Salman

Alisisitiza kuwa, utawala wa kifalme wa Aal-Saud hauna tatizo lolote na Mayahudi na kusisitiza kwamba Saudia na Israel zina mambo mengi yenye maslahi ya pamoja.

Utawala wa Aal-Saud umekuwa akisisitiza kuwa, iwapo mgogoro kati ya Israel na Palestina utapatiwa ufumbuzi, Riyadh itaimarisha uhusiano wa kibiashara wa pande mbili na Tel Aviv sambamba na kuwa na uhusiano wa kawaida.