AI: Jamii ya kimataifa ifuatilie mauaji ya mwandishi habari Msaudi
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka jamii ya kimataifa isinyamazie kimya ukandamizaji unaofaywa na serikali ya Saudi Arabia dhidi ya wapinzani wa nchi hiyo na iishinikize serikali ya Riyadh kwa ajili ya kuweka wazi faili la mwandishi habari wa nchi hiyo aliyetoweka kwa njia ya kutatanisha.
Mkurugenzi wa Utafiti wa Amnesty International kanda ya Mashariki ya Kati, Lynn Maalouf ametaka kufanyike uchunguzi huru kuhusu mauaji ya mwandishi habari na mkosoaji mkubwa wa serikali ya kifalme ya Saudi Arabia, Jamal Khashoggi akiwa nchini Uturuki na kwamba watu waliohusika na jinai hiyo wanapaswa kufikishwa mahakamani bila ya kujali vyeo na nafasi zao.
Lynn Maalouf amesisitiza kuwa, mauaji ya Jamal Khashoggi yanaweza kuwa tishio kubwa kwa watetezi wa haki za binadamu na wapinzani wa serikali ya Saudia katika maeneo yote ya dunia na kusema: Suala hilo linatatiza kazi ya kupata makimbilio ya amani kwa ajili ya wanaharakati wa nchi hiyo.
Mwandishi na mkosoaji mkubwa wa siasa za utawala wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi alitekwa nyara tarehe 2 Oktoba akiwa ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul huko Uturuki na kanali ya televisheni ya Qatar imetangaza kuwa, maiti ya Khashoggi imeokotwa katika vitongoji vya mji huo.
Jina la Jamal Khashoggi lilikuwa katika orodha ya watu wanaosakwa kwa udi na uvumba na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman na kwa msingi huo wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanasema kuwa ametekwa nyara kwa amri ya Bin Salman.