RSF: Saudia imewateka nyara wanahabari 15 mwaka mmoja uliopita
(last modified Thu, 11 Oct 2018 02:29:29 GMT )
Oct 11, 2018 02:29 UTC
  • RSF: Saudia imewateka nyara wanahabari 15 mwaka mmoja uliopita

Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka RSF limesema waandishi habari wasiopungua 15 raia wa Saudi Arabia ima wamekamatwa na vyombo vya usalama vya Riyadh au kutoweka katika mazingira ya kutatanisha katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Katika taarifa yake jana Jumatano, shirika hilo limesema aghalabu ya waandishi habari hao wa Saudia walikamatwa na maafisa usalama, lakini wao wenyewe na hata familia zao hazijui wamekamatwa kwa makosa gani au wanazuiliwa wapi.

Shirika hilo la kutetea uhuru wa waandishi wa habari duniani limewataja baadhi ya waandishi wa habari mashuhuri wa Saudia waliotoweka mikononi mwa maafisa usalama wa Aal-Saud kama Saleh al-Shihi, Essam al-Zamel, Turad al-Amri na Fayez bin Damakh. 

Jamal Khashoggi

Hii ni katika hali ambayo, asasi za kisiasa na kisheria za kimataifa na kadhalika nchi tofauti za dunia zimeendelea kulaani mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi mashuhuri wa habari na mpinzani wa utawala wa Aal-Saud, katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki.

Kwa mujibu wa takwimu za RSF, Saudia inawazuilia wanahabari na wanablogu wakosoaji wa utawala wa Riyadh kati ya 25 na 30.

 

Tags