Waqatari wapinga kuhuishwa uhusiano na utawala wa Kizayuni
Makundi mbalimbali ya wananchi wa Qatar yametangaza kuwa yanapinga kuhuishwa uhusiano wa nchi yao na utawala wa Kizayuni wa Israel sambamba na kushuhudiwa harakati za baadhi ya nchi za Kiarabu za kutaka kuhuisha uhusiano na utawala huo wa Kizayuni.
Baadhi ya wanaharakati wa masuala ya kijamii wa Qatar wametangaza kupinga kitendo cha Abu-Dhabi cha kuwa mwenyeji wa timu ya judo ya utawala wa Kizayuni. Miri Regev Waziri wa Michezo wa utawala wa Kizayuni juzi Ijumaa aliwasili Abu-Dhabi; na hiyo kuwa safari ya kwanza kufanywa na waziri wa Israel huko Imarati. Khatibu wa Sala ya Ijumaa wa Qatar huko Doha pia amekosoa kitendo cha Abu-Dhabi cha kuwa mwenyeji wa timu ya judo ya utawala wa Kizayuni.
Wakati huo huo vijana kadhaa wa Qatar wametuma barua kwa Shirikisho la Mchezo wa Judo la Qatar ambapo wamesema wanapinga Doha kuwa mwenyeji wa wanamichezo wa Israel na kusisitiza kuwa wanamichezo hao hawapaswi kukaribishwa katika ardhi ya Qatar. Aidha Wakili Mohammad Fahad al Qahatani ameandika kuwa: Kuhuisha uhusiano na utawala wa Kizayuni ni suala linalopingwa na taifa la Qatar kwa hali yoyote ile na kwamba wanaitaka serikali isitekeleza hatua hiyo. Jitihada za Imarati na baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia za kutaka kuhuisha uhusiano na utawala wa Kizayuni zinajiri katika hali ambayo ni miaka kadhaa sasa utawala huo unayakalia kwa mabavu maeneo mengi ya Kiarabu na Kiislamu mbali na kuwakandamiza raia wa Palestina.