"Uingereza ni mshiriki wa jinai za Saudi Arabia nchini Yemen"
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i49108-uingereza_ni_mshiriki_wa_jinai_za_saudi_arabia_nchini_yemen
Mbunge mmoja mwandamizi wa Uingereza amesema kuwa serikali ya nchi hiyo ni mshiriki wa jinai za Saudi Arabia dhidi ya wananchi wa Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 29, 2018 01:08 UTC

Mbunge mmoja mwandamizi wa Uingereza amesema kuwa serikali ya nchi hiyo ni mshiriki wa jinai za Saudi Arabia dhidi ya wananchi wa Yemen.

Gazeti la The Independent la nchi hiyo limemnukuu Keith Vaz, mkuu wa kundi la wabunge wa vyama vyote vya Uingereza akisema hayo na kuongeza kuwa, kitendo cha London cha kuendelea kuipa Saudi Arabia silaha na zana za kivita licha ya kwamba Riyadh inaongoza vita dhidi ya Yemen na kuua maelfu ya raia wa nchi hiyo katika kampeni zake za mashambulizi ya uwagaji wa damu ya anga, kinaifanya Uingereza kuwa mshiriki wa jinai na uhalifu huo.

Amesema, inasikitisha sana kuona kuwa licha ya kufanyika jinai na uhalifu mkubwa nchini Yemen wananchi wa nchi hiyo wamesahauliwa na hata misaada ya kibinadamu kwa nchi hiyo nayo imepungua licha ya wananchi wake kuwa katika hali ngumu sana.

Saudia inatumia silaha inazopewa na nchi za Magharibi ikiwemo Uingereza kufanya jinai dhidi ya wananchi madhlumu wa Yemen

 

Aidha amesema kuwa mauaji ya mwandishi Jamal Khashoggi yaliyofanywa na Saudia katika ubalozi wake mdogo huko Istanbul Uturuki ni ya kinyama na kikatili mno na kuongeza kuwa, Khashoggi ni mtu moja tu wakati ambapo kuna makumi ya maelfu ya watu wengine nchini Yemen wameuliwa na Saudi Arabia huku serikali ya Uingereza ikishindwa kuchukua hatua yoyote.

Mwanachama huyo mwandamizi wa chama cha Leba cha Uingereza amesema kuwa, uchunguzi unaonesha kwamba karibu asilimia 40 ya wananchi wa Uingereza hawana taarifa za jinai zinazoendelea nchini Yemen hivyo kuna haja ya kuwaamsha wananchi wa Uingereza na kuwaonesha jinsi viongozi wa nchi yao wanavyoshiriki katika jinai wanazofanyiwa wananchi wa Yemen.