Wakimbizi zaidi ya milioni moja warejea makwao nchini Syria
Wakimbizi wa Syria zaidi ya milioni moja wamerejea majumbani mwao baada ya amani na utulivu kurejea katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.
Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa serikali ya Syria ameeleza kuwa, raia karibu milioni moja na laki saba wa nchi hiyo wamerejea katika makazo yao baada ya hali ya utulivu kurejea katika miji kadhaa ya nchi hiyo. Afisa huyo wa serikali ya Syria amesisitiza kuwa, serikali inaendelea kufanya juhudi za kurejesha amani kamili nchini humo. Wakati huo huo Wizara ya Ulinzi ya Syria imetangaza kuwa marubani wawili wa Russia wameaga dunia baada ya ndege moja ya jeshi la nchi hiyo kuanguka magharibi mwa mkoa wa Homs katikati mwa Syria.
Kwingineko, ikiwa ni katika kukaribia kufanyika duru mpya ya mazungumzo ya Geneva ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa Syria, Stephen de Mistura Mjumbe, Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya nchi hiyo amewasili Tehran kwa ajili ya mazungumzo na viongozi wa Iran. Baada ya kuwasili Tehran hii leo, de Mistura alifanya mazungumzo na Hussein Amir Abdulhahiyan Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya nchi za Kiarabu na Afrika. Amir Abdullahiyan amesema amefurahishwa na kuingia katika marhala mpya mchakato wa mazungumzo ya kisiasa kati ya serikali na makundi ya wapinzani wa Syria. Naye Stephen de Mistura amesema kuwa kufanya mashauriano na viongozi wa Iran ni jambo lenye umuhimu na lenye taathira.